• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Sumu hatari zimeachiliwa ndani ya Mto Athi, bunge laelezwa

Sumu hatari zimeachiliwa ndani ya Mto Athi, bunge laelezwa

NA MARY WANGARI

BUNGE la Kitaifa limeanzisha uchunguzi kuhusiana na uchafuzi uliokithiri kwenye chemchemi muhimu za maji nchini huku ikidaiwa kwamba Mamlaka ya Kuhifadhi Mazingira Nchini (Nema) ni jibwa lisilo na meno.

Wakenya sasa wanakabiliwa na hatari ya kupata matatizo sugu ya kiafya kutokana na uchafu wa kila aina unaoachiliwa kwenye mito na mabwawa nchini, hali inayolinganishwa na shambulio la ugaidi kupitia mazingira.

Haya yamejiri kufuatia ripoti iliyowasilishwa Bungeni inayoashiria Mto Athi katika Kaunti ya Machakos na Bwawa la Thwake katika Kaunti ya Machakos kama miongoni mwa chemchemi za maji zilizoathirika zaidi kutokana na uchafuzi nchini.

Kamati ya Bunge inayoshughulikia Malalamishi ya Umma mnamo Agosti 24, 2023, ilielezwa kuwa maji katika Mto Athi na Bwawa la Thwake yamegeuzwa sumu inayoweza kusababisha maradhi.

Aidha, kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kitui Mashariki Nimrod Mbai ilielezwa kuwa, kemikali zinazomwagwa kwenye chemichemi hizo zinamechangia kuongezeka pakubwa kwa vifo kutokana na saratani nchini.

Akijibu maswali mbele ya Kamati hiyo, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alisema tafiti kadhaa zilizofanywa na wasomi nchini zimethibitisha kuwepo kwa kemikali na madini yenye sumu katika Mto Athi.

“Tafiti mbalimbali zimefanywa katika viwango vya Uzamili na Uzamifu na kwa hakika matokeo yake si mazuri. Mto Athi umechafuliwa kupindukia na huenda unaathiri afya ya watu,” alisema waziri Kindiki.

“Tunakondolea macho tatizo sugu. Baadhi ya kemikali zilizopatikana kwenye Mto Ardhi ni sumu inayowezwa kupitishwa kupitia mkondo wa chakula baina ya viumbe na kuridhishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.”

Huku akitaja uchafuzi wa chemchemi za maji nchini kama ‘ugaidi wa kimazingira’, waziri Kindiki alitoa ilani kwa mashirika ya mabwenyenye yanayomwaga uchafuzi kwenye mito na kusababishia Wakenya maafa.

Aidha, alisema Kitengo Kipya cha Polisi kilichobuniwa kwa lengo la kulinda miundomsingi ya maji kitafanyiwa mageuzi ili kujumuisha ulinzi wa chemichemi za maji nchini.

Hata hivyo, waundasheria wakiongozwa na Mbunge wa Kuria Mashariki Kitayama Marwa waliibua maswali kuhusu walichotaja kama Nema kumalizwa nguvu ya kupambana na masuala yanayohusu uharibifu wa mazingira huku hadhi yake ikidunishwa kabisa.

“Kenya imekuwa mstari wa mbele lakini sasa inakimbia majukumu yake. Tulipomwalika mkurugenzi wao hakutaka kuja na hata sikumbuki kama aliitikia wito wetu hatimaye. Mwakilishi wake alitueleza walipoteza mamlaka kitambo. Wamesalia kibogoyo. Mamlaka yametwaliwa na taasisi nyinginezo za watu wenye hela,” alisema Bw Marwa.

Kulingana naye, “Nema imegeuzwa kijisehemu tu katika orodha ambapo hata wadau katika sekta ya ujenzi wanatilia maanani zaidi Mamlaka ya Kitaifa kuhusu Ujenzi (NCA) bila kujishughulisha na Nema.”

Ilibainika vilevile katika Kaunti yote ya Machakos inayojumuisha Mlolongo, Masinga na Katani ambapo kuna mashirika anuai ya maji kama vile Mavoko Water, Warma, EPZA, “kuna maafisa wawili pekee wa Nema ambao hawana magari wala raslimali za kutosha.”

  • Tags

You can share this post!

Waziri Nakhumicha ahimiza wazazi kuhakikisha watoto...

Magaidi wa Al-Shabaab wazidiwa nguvu na walinzi wa Kenya...

T L