• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 8:50 AM
Supkem kutoa orodha ya maajenti wa safari za kwenda Hija

Supkem kutoa orodha ya maajenti wa safari za kwenda Hija

NA CECIL ODONGO

BARAZA Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM) linatarajiwa mnamo Jumapili, kutoa orodha ya maajenti halali kuwashughulikia mahujaji kwenye ibada ya Hajj mwaka huu.

Mwenyekiti wa Supkem Hassan Ole Naado alieleza Taifa Leo kwamba ukaguzi wa majina ya maajenti yaliyowasilishwa kwa baraza hilo tangu Februari 3, unatarajiwa kufanyika Jumamosi hii. Hii ni baada ya makataa ya kuwasilisha stakabadhi hitajika kukamilika siku ya Ijumaa.

Afisa huyo alisema maajenti wapya watatakiwa kusajili upya kampuni zao kulingana na kanuni zinazoongoza shughuli nzima ya ibada ya Hajj.

Hata hivyo, maajenti ambao wamekuwa wakishiriki biashara inayohusiana na safari hizo wataruhusiwa kuendelea kuhudumu baada ya kutimiza kanuni za usajili.

“Tulitoa mwanya kwa maajenti wajisajili upya na tutakagua orodha hiyo ili kuwaondoa wale ambao walihusika na ukora au ulaghai wa mahujaji mwaka jana au miaka ya nyuma. Maajenti watakaokuwa kwenye orodha itakayotolewa ndio wataruhusiwa kujihusisha na masuala ya Hajj,” akasema Bw Naado.

Kwa mujibu wa afisa huyo hakutakuwa na mwanya wa kukata rufaa kwa maajenti ambao watakosa kuidhinishwa na watalazimika wasubiri hadi mwaka ujao ili kutuma maombio upya.

Maajenti wamekuwa wakituma stakabadhi ili kutimiza agizo jipya la Supkem la kuhakikisha wale ambao wanatambuliwa pekee ndio wanahusika na safari za Hijja.

Mwaka uliopita, kulizuka malalamishi ya baadhi ya mahujaji kwamba maajenti wao walikosa kuhakikisha wanapata pasipoti kwa wakati.

You can share this post!

Serikali yalaumiwa kusaliti Mau Mau, familia ya Kimathi

Serikali yataka maoni ya Wakenya kuhusu Sheria ya Data

adminleo