• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Swazuri ajitapa huduma yake NLC imeleta ‘ufanisi mkubwa’

Swazuri ajitapa huduma yake NLC imeleta ‘ufanisi mkubwa’

MOHAMED AHMED na WACHIRA MWANGI

MWENYEKITI wa Tume ya Ardhi Nchini (NLC) Muhammad Swazuri amesema kuwa anamaliza awamu yake kwenye tume hiyo akiwa mwenye furaha.

Prof Swazuri ambaye amekumbwa na masaibu akiwa afisini na kashfa za ufisadi alisema kuwa wakati awamu yake ikimalizika, haoni sababu ya kujuta kutopewa nafasi ya kufanya kazi na makamishna wenza.

Alisema hilo ni kwa sababu yalikuwa ni maamuzi ya mahakama. Akizungumza wakati alipokuwa anatoa ripoti kuhusiana na umiliki wa ardhi za Mombasa kisiwani katika ukumbi wa Tononoka, Prof Swazuri alisema masaibu ambayo amekuwa akikumbana nayo yameletwa na “vidudu watu” ambao hawana raha na kazi yake.

“Nimekuwa nikienda kwenye ofisi zote. Kile kilichonizuia kutofanya kazi na makamishna wenzangu ni amri ya korti na sio maaumizi yangu. Wakati namaliza awamu yangu nitajivunia kwani nimetatua shida za wengi na nitatembe bila uoga wowote,” akasema Prof Swazuri.

Alisema kuwa anaridhika kuwa vyombo vya habari vimempa umaarufu si haba na hajutii hilo.

Alidai kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimelipwa kuchafua jina lake na watu aliosema kuwa ni wezi wa ardhi za umma.

Vyombo vya habari vimekuwa vikimmulika Prof Swazuri kwa sababu ya kashfa za ufisadi na utumizi mbaya wa afisi yake.

Aidha, jana Prof Swazuri alisema kuwa tume hiyo ya NLC chini ya usimamizi wake imetekeleza ya kutosha kutatua shida za wakazi wa maeneo tofauti humu nchni.

“Tungekuwa na rasilimali ya kutosha basi tungekuwa tumefanya kila kitu kama ipaswavyo kisheria lakini kama mujuavyo kuna mambo mengi, hata hivyo licha ya hayo tumetekeleza ya kutosha. Tunapigwa vita kwa sababu ya uwezo wa tulionyesha kutekeleza mengi,” akasema.

Prof Swazuri alisema kuwa chini ya uongozi wake ameweza kutekeleza mazuri ambayo wizara ya ardhi ilishindwa kufanywa kwa muda wa miaka 100.

“Najua kuwa tumetoa maelfu ya hati miliki. Tumeweza kutekeleza miradi ya 81 ya serikali ndani ya miaka hii minne jambo ambalo wengine walishindwa kufanya kwa miaka 100,” akaongeza.

Alitoa mifano ya baadhi ya yale tume hiyo imeweza kutekeleza na kuuliza mbona mambo hayakutekelezwa, “kwani hakukuwa na wizara kabla ya kuja kwa NLC?”

Miongoni mwa mifano aliyotoa ni pamoja na suala la utata wa ardhi ya Waitiki eneo la Likoni, Maili Tisa na mengine mengi nchini kote.

“Tumepigana na kutatua shida za dhuluma za ardhi za kihistoria ambazo zimekuwa hapa katika kanda ya Pwani. Tumetatua kesi zaidi ya 262 ambazo hazikuwa zimetatuliwa hapo awali,” akasema Prof Swazuri.

Alisema yeye haangalii kupata umaarufu na lengo kuu ni kuhudumia wananchi wa Kenya.

Alisema kuwa kiongozi mzuri ni yule ambaye wakati mwengie atagombana na watu na kuongeza, “Naondoka nikiwa na furaha na kama unataka umaarufu basi nenda ukauze aisikirimu.”

Alisema kuwa hakuna yoyote ambaye anaweza kutatua shida za ardhi kwa pamoja na kuongeza kuwa suluhu moja linaleta shida kwengine.

Prof Swazuri pia aliwatakia heri maafisa wapya ambao watakuwa wanaingia afisini baada ya kuondoka kwa kikosi chake.

You can share this post!

Hospitali yajitetea kuhusu mama kubeba mtoto mfu hadi...

Waumini wamkataa askofu mpya

adminleo