• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Uislamu si dini ya kigaidi, wanafunzi wahamasisha wenzao

Uislamu si dini ya kigaidi, wanafunzi wahamasisha wenzao

NA STEVE MOKAYA

Muungano wa Wanafunzi Waislamu (MWW) katika Chuo Kikuu cha Mombasa (TUM) uliandaa shughuli ya kuhamasisha umma kuhusu dini hiyo Jumatano.

Shughuli hiyo ya kila mwaka na inayochukua siku mbili ilianza Jumatano asubuhi, katika ukumbi wa mahafala wa chuo hicho.

Wanafunzi Waislamu walichukua nafasi hiyo kuwahamasisha wanafunzi wenzao ambao sio Waislamu kuhusu ukweli halisi wa dini lao.

Kulingana na Said Hassan, ambaye ni mwenyekiti wa muungano huo, vyombo vya habari, hasa vya mataifa ya kigeni vimepotosha ulimwengu kuwa Uislamu ni dini ya ugaidi.

Aliongeza kuwa hamasisho hilo lililenga kuwaambia watu ukweli wa mambo kuhusu hadhi ya wanawake katika Uislamu.

Uisilamu si ugaidi. Picha/ Steve Mokaya

Bw Hassan, katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali, alisema kuwa Uislamu hauungi mkono wala kufunza itikadi kali kamwe. Alieleza kuwa wale majambazi wanaoshiriki ugaidi na kujificha chini ya mwavuli wa Islamu sio waislamu halisi.

“Mungu, kupitia kwa Quran takatifu, anatufunza kuheshimu maisha ya binadamu, wala hakuna yeyote aliyepewa mamlaka ya kumwua mwingine,” alieleza.

Kuhusu haki za wanawake katika dini ya Uislamu, Bw Hassan alisema kuwa ni uongo mtupu watu kusema kuwa dini yao hudharau wanawake na kuwashusha hadhi katika jamii.

Alieleza kuwa Quran inafunza Waislamu kuwaheshimu wanawake na kuwapa haki zao kikamilifu.

Charity Buyabo afurahia Quran Takatfu. Picha/ Steve Mokaya

“Quran iko na sura nzima inayozungumzia kuhusu jinsi wanawake wanapaswa kutunzwa na kuheshimiwa. Kadhalika, kunayo sura ingine iliyopewa jina la Maria, ambaye ni mamake Yesu. Uislamu unamtambua Maria kama mama wa hadhi ya juu zaidi ulimwenguni,” Bw Hassan alieleza.

Katika uhusiano wa Ukristo na Uislamu, alisema kuwa Waislamu wanawapenda sana Wakristo, maana dini zote mbili zinamtambua na kumpenda Yesu.

Mafundisho ya dini hizo mbili yanakaribiana sana. “Sote tunaamini kuwa Yesu yuko. Tofauti ni kwamba Wakristo huamini kuwa Yesu ni Mungu; na sisi tunaamini kuwa Yesu ni nabii wa Mungu. Aidha sisi huamini kuwa Muhammed ndiye mtume mkuu na wa mwisho aliyetumwa na Mungu na kuleta Quran takatifu. Hatuna uadui kamwe,” alifafanua.

Bw Hassan akiwa na wenzake chuoni TUM. Picha/ Steve Mokaya

Shughuli hiyo iliwavutia wanafunzi mbalimbali, wavulana kwa wasichana, na hata wafanyakazi wa chuo hicho cha Mombasa.

Waliohudhuria walipewa elimu kuhusu Uislamu na wanafunzi Waislamu, pamoja na kujibiwa maswali waliyokuwa nayo.

Mbali na kupewa mafunzo ya moja kwa moja kupitia kwa maneno ya mdomo, pia walipewa vitabu mbalimbali vya Kiislamu, kikiwemo Quran.

Waislamu wanampenda Yesu Kristo. Picha/ Steve Mokaya

Bi Anita Kasuku, mwanafunzi wa mwaka wa tatu, ambaye ni Mkrsisto Mwadventista, alihudhuria na kupokezwa mafunzo na ufafanuzi.

“Rafiki yangu tunayesoma naye darasni alinikaribisha huku, na nikaja. Nimepewa maelezo kadhaa kuhusu Uislamu, na pia nikapewa vitabu na majarida ya kusoma. Pia nimepewa Quran, na nitaenda kusoma ili nijue uhusianao kamili uliopo,” alieleza.

Shughuli hiyo itatamatika Alhamisi.

Anita Kasuku aonyesha Quran Takatifu. Picha/ Steve Mokaya

You can share this post!

Maafisa wa voliboli Misri wachunguzwa

Watu 11 waliofaidi kutokana na utawala wa Mzee Moi

adminleo