• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
UJASIRIAMALI: Agundua siri kupunguza gharama ya juu ya chakula cha mifugo  

UJASIRIAMALI: Agundua siri kupunguza gharama ya juu ya chakula cha mifugo  

NA SAMMY WAWERU

GHARAMA ya ufugaji nchini inazidi kuwa ghali kutokana na mfumko wa bei ya chakula cha mifugo cha madukani.

Ongezeko hilo limechangiwa na kuendelea kukosekana kwa malighafi yanayotumika kukitengeneza, hasa janga la corona lilipotua Kenya 2020.

Isitoshe, yanayopatikana hayakamatiki kufuatia ushuru wa juu unaotozwa.

Huku wengi wakilemewa kuendeleza ufugaji, Cosmas Mutiso mfugaji wa ng’ombe wa maziwa Kaunti ya Makueni hahisi gharama hiyo.

Akiwa na ng’ombe wanane anaokama maziwa, sita ambao hawajajiunga na mtandao wa uzalishaji na fahali mmoja, mfugaji huyu wa Kijiji cha Kanaani, Kibwezi amegundua siri kushusha gharama.

Matawi na majani ya mtama, Mutiso anayatumia kutengeneza malisho; silage na hay.

Katika mradi wake, ana eneo maalum (shimo) la shughuli hiyo. Mitama, almaarufu ‘miwa ya jangwani’, huvuna ikiwa na miezi miwili baada ya upanzi.

“Inapoanza kuchana maua, huivuna,” asema, akidokeza kwamba amekodi ekari tatu karibu na Mto Kiboko kuilima.

Katika umri huo, mitama ina asilimia 15 ya Protini kiwango ambacho ni cha juu mno kikilinganishwa na cha chakula kingine.

Cosmas Mutiso, mwasisi wa Kanaani Dairy Farm Makindu akielezea aina bora ya mtama kutengenezea silage na hay. PICHA | SAMMY WAWERU

Huipa muda wa saa 24, ili kupunguza kiwango cha maji, kisha anaisaga kwa kutumia mashine aina ya chaff cutter.

Aidha, ana mashine mbili zinazotumia mafuta ya petroli na dizeli.

Vipande vilivyosagawa, huviweka kwenye mifuko ya nailoni iliyofungwa kutoruhusu hewa yoyote ile kuingia.

Vilevile, huambatanisha na molasi, na kuwekwa kwenye shimo linalofunikwa kwa karatasi ngumu ya nailoni.

“Hufunika juu kwa udongo, na kuruhusu malisho yachache,” Mutiso aelezea. Inachukua kipindi cha mwezi mmoja silage kuwa tayari.

“Kiwango cha virutubisho vyake ni cha juu, kikilinganishwa na hay.”

Hay, mitama anayokausha, huipiga jeki kwa nyongeza kama maize germpollard na chakula cha madukani.

Mwasisi huyu wa Kanaani Dairy Farm Makindu, anasema kwa kujiundia malisho amepunguza gharama ya ufugaji kwa asilimia 40.

Aliingilia ufugaji wa ng’ombe wa maziwa 2012, baada ya kiangazi kusitisha jitihada zake kufuga wale wa kienyeji.

“Mwaka 2008 na 2009, nilipoteza mifugo wenye thamani ya Sh1.2 milioni waliokufa njaa,” afichua.

Ng’ombe wa maziwa, alianza na wawili pekee alionunua jumla ya Sh158, 000 kutoka Nyandarua.

Mfumo wa kujitengenezea chakula, Mutiso anasema alitambua kupitia mfugaji hodari aliyeukumbatia.

“Kila ng’ombe kwa sasa anatoa kati ya lita 15 – 20 kwa siku, kutoka chini ya 10,” anaiambia Akilimali Dijitali.

Mutiso pia ana kondoo 67.

Wataalamu wanahimiza wafugaji kujiundia malisho, kupitia nyasi kama vile mabingobingo, Lucerne, na matawi ya nafaka ili kupunguza gharama.

“Chakula cha kujitengenezea na kuongeza malighafi faafu na yenye virutubisho, ni bora kuliko kile cha madukani,” ashauri Michael Ngaruiya, mtaalamu mifugo.

Lita moja ya maziwa, Mutiso huuza Sh60.

Licha ya ufanisi aliopata, analalamikia gharama ya juu ya dawa za vimelea na mafuta ya petroli ikizingatiwa kuwa hutumia mashine kusaga mitama.

Alikuwa miongoni mwa wakulima waliopata fursa kuonyesha mifumo wanayotumia, katika hafla iliyoandaliwa na The International Crops Research Institute for Semi-Arid Tropics (ICRISAT), jijini Nairobi mwaka huu wa 2022.

  • Tags

You can share this post!

UFUGAJI: Wafugaji watafuta njia za kumudu gharama ya lishe

Hoki: Butali Warriors yapiga Sailors kurejea kileleni,...

T L