• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 7:55 AM
Urais: Cherargei alimwa na viongozi wa upinzani

Urais: Cherargei alimwa na viongozi wa upinzani

RUSHDIE OUDIA, MERCY SIMIYU NA COLLINS OMULO

PENDEKEZO la Seneta Samson Cherargei wa Kaunti ya Nandi kwamba muhula wa kuhudumu wa rais unafaa kuongezwa kutoka miaka mitano hadi miaka saba, limekosolewa vikali na upinzani na viongozi wengine nchini.

Bw Cherargei aliwasilisha pendekezo hilo kwa Kamati ya Mazungumzo ya Maridhiano inayoendesha vikao vyake katika Ukumbi wa Bomas, Nairobi, akishinikiza Katiba kubadilishwa ili kuongeza muhula mmoja wa rais kuhudumu kutoka miaka mitano hadi miaka saba kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, pendekezo hilo limekosolewa vikali, baadhi ya viongozi wakilitaja kuwa lisilofaa hata kidogo.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Opiyo Wandayi, alisema hakushangazwa na hatua hiyo, kwani Bw Cherargei ni mshirika wa karibu wa Rais Ruto.

Hata hivyo, alisema atafanya kila awezalo kupinga mipango hiyo.

“Hili ni jaribio tu la mipango inayoendelea. Lengo kuu ni kuondoa mihula ambayo rais anafaa kuhudumu. Lakini hawatafaulu. Wakenya watakataa,” akasema Bw Wandayi, ambaye pia ni Mbunge wa Ugunja.

Kauli yake iliungwa mkono na mwenzake Samuel Atandi (Alego Usonga), aliyesema waliona mipango hiyo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

“Huo ndio wasiwasi tuliokuwa nao, kwamba Ruto angefuata nyayo za kiimla kutoka kwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda. Amefanya hivyo tena. Imani yangu ni kuwa anamaanisha anachopanga kufanya. Anataka kuwa rais ambaye hatang’atuka uongozini,” akasema Bw Atandi.

Pendekezo hilo linajiri wakati serikali ya Kenya Kwanza inakabiliana na mivutano ya kindani baina ya viongozi wake, ukosoaji kutoka kwa raia kutokana na gharama ya juu ya maisha na kutotimizwa kwa ahadi ilizotoa wakati wa kampeni.

Seneta Moses Kajwang’ wa Homa Bay, alitaja pendekezo hilo kama njia ya kuwapumbaza Wakenya kutokana na changamoto wanazopitia.

“Hakuna Mkenya yeyote angetaka kuona muda wa mahangaiko wanayopitia ukiongezwa hata kwa siku moja na utawala wa Kenya Kwanza. Ni wazi kuwa serikali imeishiwa na mbinu za kuiongoza nchi na imeanza kubuni njia za kuwapumbaza Wakenya kutokana na changamoto wanazopitia,” akasema Bw Kajwang’.

Wakihutubu katika Shule ya Msingi ya Mungore wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya mpango wa kuwalisha wanafunzi, viongozi hao walimlaumu seneta huyo dhidi ya kupanga njama za kuirejesha nchi katika nyakati za giza.

Waliapa kupinga mipango hiyo kwa vyovyote vile kwa manufaa ya Wakenya wote.

“Yeye (Cherargei) bado anaishi katika nyakati za utawala wa Rais Mstaafu (marehemu) Daniel Moi. Watu wanateseka na yeye anatwambia kuongeza muda wa kuhudumu. Tunamwambia kuwa hilo halitafaulu. Tutakabiliana naye vilivyo,” akasema Mbunge wa Bumula, Jack Wabomba.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Museveni adai jeshi lake liliua wanamgambo

Kajala awakataa wanaume wa Kenya kwa kumchezea...

T L