• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
Utalii: Balala apingwa kuhusu ubinafsishaji

Utalii: Balala apingwa kuhusu ubinafsishaji

Na SIAGO CECE

WADAU katika sekta ya utalii wameikashifu serikali kwa kupendekeza mipango ya kuzifanya mbuga za wanyama za kitaifa kusimamiwa na mashirika ya kibinafsi.

Wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Muungano wa Wafanyikazi wa Hotelini (KAHC), Dkt Sam Ikwaye, walisema hatua hiyo inaweza ikaathiri vibaya utalii nchini.

“Ni makosa kubwa kwa serikali. Kampuni nyingi ambazo zinamilikiwa na watu kibinafsi hazileti faida yoyote kwa raia wa kawaida,” Bw Ikwaye alisema.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri wa Utalii na Wanyamapori, Bw Najib Balala alisema kuwa serikali inapanga kuweka baadhi za mbuga za wanyamapori na taasisi nyingine za kitalii zinazosimamiwa na serikali kuwa za kibinafsi.

Kulingana naye, hatua hiyo itawezesha serikali kufanya biashara bila hasara.

Alieleza kuwa janga la corona limeathiri sana sekta hiyo na ni muhimu kubadilisha mtindo wa jinsi serikali inajihusisha katika biashara kwani kumekuwa na hasara tele tangu mwaka uliopita.

“Kwa nini serikali imiliki mbuga za wanyama? Haya ndio mambo ambayo tunapaswa kubadilisha,” Bw Balala alisema katika kongamano lililoandaliwa kupitia mtandaoni.

Kando na mbuga za wanyama, serikali husimamia taasisi nyingine kama vile hoteli na vyumba vya mikutano ambavyo wadau wanahofia huenda pia ikaamuliwa zisimamiwe na mashirika ya kibinafsi.

Kulingana na Bw Ikwaye, shirika la kitaifa la ndege la Kenya Airways ni mojawapo ya kampuni za serikali ambazo zimepata changamoto nyingi baada ya kuwekwa kwa mikono ya watu binafsi.

Bw Ikwaye pia alisema mara nyingi, kampuni binafsi huenda zikadhulumu Wakenya kwa kuwatoza ada za juu kabla ya kuingia mbugani.

Alirai wizara hiyo kufanya utafiti kamili kabla kutoa msimamo ya jinsi mbuga za wanyama kumilikiwa na watu binafsi.

Kwa upande wake, afisa mkuu wa muunganio wa watalii Pwani (KCTA) Julius Owino alisema ni heri mashirika mbalimbali ya serikali yaunganishwe badala ya kuyafanya yawe ya kibinafsi.

“Mbuga za wanayamapori ni hazina kubwa ya nchi na haiwezi kupewa kwa watu binafsi, ikiwa serikali ina mipango ya kufanya hivyo, inamaanisha imeshindwa kuzihifadhi,” Bw Owino alisema.

Kenya ina mbuga zaidi ya 20 ambazo zimemilikiwa na serikali. Mapema mwezi huu serikali ilianzisha rasmi shugli ya kuhesabu wanyamapori wote nchini ili kujua idadi na kuboresha uhifadhi wa wanyama hao.

You can share this post!

Covid: Magavana zaidi katika hatari ya kuadhibiwa

Rais Biden sasa ataka Israeli isitishe mashambulio Gaza