• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:45 PM
Uzee sio uchawi, lasema shirika likikemea mauaji ya wakongwe Kisii

Uzee sio uchawi, lasema shirika likikemea mauaji ya wakongwe Kisii

NA WYCLIFFE NYABERI

Shirika la Ahadi Kenya Trust limetoa wito kwa jamii za Kenya kuwaheshimu wazee na kuwatunza vyema na sio kuwashambulia kwa kuwahusisha na ushirikina.

Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo Dkt Stanley Kamau amewataka Wakenya, haswa vijana kutilia maanani ustawi wa wazee kwa kuwapa maisha ya heshima badala ya kuwashtumu kwamba wanafanya uchawi.

Akizungumza mjini Kisii mnamo Ijumaa, Agosti 18, 2023, alipoongoza ugawaji wa vyakula na mavazi  kwa wazee huko Igare, Dkt Kamau alisema wamekuwa wakihuzunishwa na visa vya wazee kuitwa wachawi Gusii na sehemu zingine za Pwani na Kaskazini Mashariki.

Dkt Kamau aliwakashifu wakandamizaji wa wazee kwa kuwaita kila aina ya majina na kutaja tabia zao zisizo za Kimungu.

“Linapotokea jambo la bahati mbaya kwenye familia, wao (wakandamizaji) wanawakuta wakongwe na kuwaita majina ya kila aina. Hatimaye wanawaua kwa kuwateketeza moto,” Dkt Kamau alisema.

Mkurugenzi huyo alisisitiza haja ya mamlaka kuchukua hatua kali dhidi ya wale wanaowatesa wazee kama njia mojawapo ya kuzuia maovu hayo yasijirudie mara kwa mara.

Alikasirishwa na madai ya kushambuliwa kwa wazee katika nyumba ya kuwatunza wazee ya PCEA Thogoto na kusema ikiwa fichuzi iliyotolewa na shirika la habari la BBC ni kweli, basi kuna haja ya serikali kudhibiti nyumba za wazee, kuzisimamia na kuhakikisha kuwa wazee wanaishi katika maisha ya heshima.

Katika ufichuzi wa hivi majuzi, BBC ilianika unyanyasaji wa wazee katika Thogoto Care Home, na kuzua hisia kali kutoka kwa Wakenya.

Katibu Mkuu wa Ulinzi wa Jamii na Masuala ya Wazee wa Kenya, Joseph Motari, alilaani dhuluma hiyo na kuahidi hatua zinazofaa dhidi ya waliohusika.

  • Tags

You can share this post!

Wahudumu wa zamani wa NMS walia kuachwa kwa mataa

Mwanamume aliyeshtakiwa kuchafua mtoto alaumu shetani

T L