• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Vifo 174 na mahangaiko Israeli ikizidi kuwalipua Wapalestina

Vifo 174 na mahangaiko Israeli ikizidi kuwalipua Wapalestina

Na AFP

JERUSALEM, Israel

IDADI ya watu waliouawa katika mapigano kati ya Israeli na Palestina katika ukanda wa Gaza jana ilifikia 174 baada ya ndege za kivita za Israeli kuwaua Wapalestina wengine 17 Jumapili asubuhi.

Wizara ya Afya katika eneo la Gaza ilisema kuwa 47 miongoni mwa waliouawa walikuwa watoto; katika mapigano makali yaliyoanza Jumatatu wiki iliyopita. Vilevile, zaidi ya watu 1,200 wamejeruhiwa katika mapigano hayo.

Nchini Israeli, jumla ya watu 10 wameuawa kwenye msururu wa roketi zilizofyatuliwa kutoka Gaza.

Jumapili, jeshi la Israeli liliungama kuwa lilishambulia kwa mabomu nyumbani kwa kiongozi wa kundi la wapiganaji la Hamas katika eneo hilo la Gaza, wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) likitarajiwa kufanya mkutano kujadili mzozo huo.

Mashambulio ya jana, yalilenga vituo 90 katika eneo la Gaza ambapo jengo lenye afisi za mashirika ya habari ya AFP na Al Jazeera liliharibiwa Jumamosi. Kitendo hicho kililaaniwa vikali na viongozi wa kimataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres alielezea kutamaushwa na idadi kubwa ya raia waliouawa katika ukanda wa Gaza na kushambuliwa kwa jumba lenye afisi za mashirika hayo mawili ya habari ya kimataifa.

Jeshi la Israeli lilisema karibu roketi 2,900 zilirushwa kutoka ukanda huo, unaodhibitiwa na Hamas, kuelekea Israeli.

Mtambo wa Israeli wa kudhibiti makombora ulitungua roketi 1,150 ndani ya wiki moja wakati ambapo majumba ya makazi wanakoishi Waisraeli yalishambuliwa na ving’ora kulia katika miji kadhaa.

Mapigano hayo mabaya zaidi kutokea ndani ya miaka saba pia yamechochea mapigano ya kijamii na ongezeko la visa vya mashambulio ya halaiki kati ya Wayahudi na Waisraeli wa asili ya Kiarabu.

Pia yamechochea mapigano katika eneo la West Bank linalodhibitiwa na Israeli.

Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) lilisema lililenga vituo vya Hamas na kundi la Jihad, viwanda na maghala ya risasi.

Jeshi hilo lilisema ndege zake za kivita zilishambulia boma la Yahya Sinwar, ambaye ni kiongozi wa kitengo cha kisiasa cha Hamas katika ukanda wa Gaza. Lilitoa video iliyoonyesha moshi na uharibifu uliotokea lakini halifichua ikiwa kiongozi huyo wa Hamas aliuawa au la.

“Miongoni mwa vituo vilivyoshambuliwa ni makazi ya Yahya Sinwa, Mwenyekiti wa Kituo cha Kisiasa cha Hamas eneo la Gaza, pamoja na kakake, Muhammad Sinwar, Mkuu wa Idara ya Uchukuzi na Ajira katika kundi la Hamas,” jeshi la Israeli lilisema kwenye taarifa.

  • Tags

You can share this post!

MAYATIMA WA BBI

HAWA LEICESTER: Bao la Youri Tielemans kwenye fainali...