• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Fahamu vikosi 13 kati ya 32 ambavyo tayari vimefuzu kwa Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar

Fahamu vikosi 13 kati ya 32 ambavyo tayari vimefuzu kwa Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar

Na MASHIRIKA

MWAKA mmoja kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar kupulizwa, baadhi ya mataifa tayari yamejikatia tiketi za kunogesha kipute hicho.

Vikosi vingine kutoka bara Ulaya na Afrika vitasubiri hadi kukamilika kwa mchujo wa Machi ili kujiunga na timu 13 kati ya 32 ambazo tayari zimejikatia tiketi za kuelekea Qatar.

Mbali na wenyeji Qatar, timu nyinginezo ambazo zimefuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022 ni Ubelgiji, Uingereza, Uhispania, Croatia, Ujerumani, Uswisi, Denmark, Uholanzi, Brazil, Serbia, Argentina na mabingwa watetezi Ufaransa.

Timu za bara Ulaya ambazo lazima zishiriki mchujo mnamo Machi 24-25, 2022 kabla ya kufuzu ni Wales, Scotland, Italia, Ureno, Uswidi, Urusi, Poland, Macedonia Kaskazini, Uturuki, Ukraine, Jamhuri ya Czech na Austria.

Mbali na Argentina na Brazil, timu nyinginezo zinazopigiwa upatu wa kufuzu kutoka Amerika Kusini ni Ecuador na Colombia huku Canada, Amerika na Mexico zikitarajiwa kusonga mbele kutoka Amerika Kaskazini, Amerika ya Kati na Caribbean.

Wawakilishi wa bara Asia wanatazamiwa kuwa Japan, Australia na Saudi Arabia kutoka Kundi A pamoja na Iran na Korea Kusini wanaokamilisha Kundi B linalojumuisha pia wenyeji Qatar.

Afrika itawakilishwa na vikosi vitano vitakavyoshiriki mchujo wa mikondo miwili mnamo Machi 2022. Vikosi hivyo ni 10 vilivyoibuka vya kwanza katika raundi ya kampeni za makundi. Navyo ni Misri, Algeria, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ghana, Mali, Morocco, Nigeria, Senegal na Tunisia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kune Food kutumia teknolojia kuwalisha Wakenya vyakula vya...

Red Carpet inataka miaka minne ili kutinga ligi kuu ya FKF...

T L