• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Wazungu wapapasa Raila mgongo

Wazungu wapapasa Raila mgongo

LEONARD ONYANGO Na JUSTUS OCHIENG

HATUA ya kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga kufifisha mapambano dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza imezua maswali tele huku wadadisi wakisema kuwa mataifa ya kigeni yamechangia kumnyamazisha.

Bw Odinga alikuwa ameahidi kutangaza mikakati yake ya kuanzisha mapambano dhidi ya serikali ya Rais William Ruto mwezi huu, lakini angali kimya.

Bw Odinga ameonekana kupunguza kasi ya mapambano tangu alipoahirisha ghafla mkutano mbadala wa Upinzani uliofaa kufanyika uwanjani Jacaranda jijini Nairobi kuadhimisha sherehe za Jamhuri mnamo Desemba 12, mwaka jana.

Mkutano huo ambao Bw Odinga alikuwa ameutaja kuwa mwanzo wa mapambano dhidi ya serikali ya Rais Ruto, ulifutiliwa mbali siku mbili kabla ya Decemba 12.

Bw Odinga aliambia wafuasi wake kuwa alialikwa kwenye kongamano la viongozi wa Afrika na Amerika lililofanyika jijini Washington DC kati ya Desemba 13 na 15.

“Tumeahirisha mkutano wa Jacaranda kwa sababu nilialikwa na Rais wa Amerika Joe Biden kuhudhuria kongamano. Wakenya wafahamu kuwa sijatishwa na serikali. Mimi si mtu wa kutishwa,” alisema Bw Odinga kabla ya kuelekea jijini Washington DC.

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Rais William Ruto lakini haijulikani ikiwa wawili hao walikutana faraghani. Aidha, haijulikani ikiwa Bw Odinga alikutana na Rais Biden au maafisa wakuu wa serikali ya Amerika.

Lakini tangu aliporejea nchini kutoka Amerika, Bw Odinga amekuwa akikutana na mabalozi wa nchi mbalimbali za Magharibi.

Jumatano, Bw Odinga alikutana na Balozi wa Uingereza humu nchini, Bi Jane Marriott, katika ubalozi wa Uingereza.

Bw Odinga aliyekuwa ameandamana na aliyekuwa gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na Katibu Mkuu wa Azimio Junet Mohamed, alifichua kuwa walijadili masuala nyeti humu nchini.

“Tuliafikiana kwamba tutakuwa tukishauri ubalozi wa Uingereza kuhusiana na masuala ya nchi hii mara kwa mara,” akasema Bw Odinga.

Bi Marriott kwa upande wake, alimiminia Bw Odinga sifa tele huku akimtaja kama kinara wa masuala ya demokrasia nchini.

Balozi Marriott alifichua kuwa suala kuhusu namna ya kuendesha upinzani ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa.

Mkutano huo wa Jumatano ulifanyika siku 20 tu baada ya Bw Odinga kukutana na Balozi wa Ujerumani humu nchini Sebastian Groth.

Baada ya mkutano huo, Bw Odinga alisema kuwa alimtaka Bw Groth kuhimiza Ujerumani ‘kufungulia milango’ Wakenya wanaosaka fursa katika taifa hilo la Ulaya.

Wadadisi wanabashiri kuwa mikutano hiyo huenda inalenga kumshawishi Bw Odinga kutumia mbinu mbadala za kukosoa serikali badala ya maandamano na mikutano ya kisiasa.

Jumatano, Bw Odinga alikutana na viongozi kutoka maeneo ya Nyanza na kuwahimiza kumpokea Rais Ruto ambaye leo anazuru Kaunti ya Homa Bay na kesho Kaunti ya Siaya.

Rais Ruto atalakiwa na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga ambaye alimkwepa Oktoba mwaka jana Kiongozi wa Nchi alipozuru kaunti hiyo.

Bw Odinga Jumatano alikutana na viongozi kutoka kaunti hizo mbili akawambia wampokee kwa mikono miwili Rais Ruto kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Mbunge wa Rangwe Dkt Lilian Gogo jana aliambia Taifa Leo kuwa waliafikiana katika mkutano wa Jumatano kuwa viongozi waliochaguliwa katika eneo la Nyanza ndio watakuwa wenyeji wa Rais Ruto.

“Tuliagizwa na kiongozi wetu wa chama (Bw Odinga) kuwa twende tumlaki Rais Ruto,” akasema Dkt Gogo.

Bw Oparanya ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa ODM, aliambia Taifa Leo kuwa chama kiliwapa ruhusa viongozi wa Nyanza kumpokea Rais Ruto.

Bw Odinga tayari ameidhinisha magavana wa Azimio kushirikiana na Rais Ruto kwa ajili ya maendeleo katika kaunti zao.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa Rais Ruto, jana alisema kuwa Kiongozi wa Nchi yuko huru kuzuru Nyanza.

“Watu wa jamii ya Waluo ni wakarimu. Tunapenda demokrasia,” Bw Wandayi ambaye yuko ziarani nchini Amerika akaambia Taifa Leo.

Bw Javas Bigambo, mdadisi wa masuala ya kisiasa, anasema kuwa japo kuna uwezekano kwamba mataifa ya kigeni yamehusika katika kupoza Bw Odinga, kinara wa Upinzani amepunguza kasi ya mapambano baada ya kukosa kuungwa mkono.

“Bw Odinga alianzisha mapambano akijua kuwa angeungwa mkono na wandani wake lakini wengi wao wamemhepa. Aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho, kwa mfano, amejitenga na Bw Odinga. Magavana wa Azimio wametangaza kushirikiana na Rais Ruto,” asema Bw Bigambo.

“Hivyo, Bw Odinga ameonekana mpweke na hivyo hana jingine bali kuunga mkono Rais Ruto.”

  • Tags

You can share this post!

DRC yakemea Rwanda kuwakataa wakimbizi

Viungo vya kujitengenezea vinavyodhuru ngozi yako baada ya...

T L