• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
‘WHO haitaishinikiza Uchina kufichua chanzo cha corona’

‘WHO haitaishinikiza Uchina kufichua chanzo cha corona’

NA MASHIRIKA

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limesema haliwezi kuilazimisha Uchina kutoa habari zaidi kuhusu chanzo cha Covid-19.

Aidha, WHO imesema kuwa itapendekeza tafiti zinazohitajika ili kuongeza “kiwango” cha ufahamu kuhusu asili ya virusi hivyo.

“WHO haina mamlaka ya kumshurutisha yeyote kuhusu suala hili,” alisema Mkurugenzi wa Shirika hilo anayesimamia idara ya dharura Mike Ryan.

Afisa huyo alisema hayo Jumatatu wakati wa mahojiano na vyombo vya habari kuhusu mipango ya WHO ya kuishinikiza Uchina kuwa na uwazi zaidi.

“Tunatarajia ushirikiano kikamilifu, kujitolea na kuungwa mkono na mataifa ambayo ni wanachama wetu kuhusu suala hilo,” alisema Ryan.

Kuna dhana kadhaa kinzani zinazosema kuwa virusi hivyo viliruka kutoka kwa wanyama hususan popo na kuwaingia binadamu au kuwa virusi hivyo vilisambaa kutoka maabara moja mjini Wuhan, Uchina.

Nadharia ya ‘kuvuja kutoka lebu Wuhan’ imegeuka mjadala mkali kwa mara nyingine katika siku za hivi karibuni baada ya wanasayansi kadhaa maarufu kuitisha uchunguzi kamili kuhusu asili ya virusi hivyo.

Makisio kuwa virusi hivyo vilivujwa kwa bahati mbaya kutoka kwa lebu yalipuuziliwa pakubwa na wanasayansi katika hatua za kwanza za mkurupuko wa virusi vya corona.

Uchina imekanusha kila mara kwamba, lebu hiyo ndiyo iliyosababisha mkurupuko huo.Timu ya WHO iliyozuru Uchina mapema mwaka huu ikisaka chanzo cha Covid-19 ilisema kuwa hawakuweza kupata data yote hivyo kuzidisha mjadala kuhusu uwazi wa taifa hilo.

Aliyekuwa rais wa Amerika, Donald Trump na wafuasi wake wamekuwa wakisisitiza dhana kuwa Uchina ilisambaza virusi hivyo kimaksudi.

Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Amerika Mike Pompeo alisisitiza mwaka jana kwamba kuna “ushahidi thabiti” kuwa virusi hivyo vilitoka kwenye lebu, huku akikosa kutoa ushahidi wowote na kukiri kwamba hakukuwa na uhakika.

Wakati huo huo, kinara wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ametoa wito kwa kampuni zinazounda chanjo za Covid-19 kupatia mradi wa kimataifa unaolenga kuleta usawa kuhusu chanjo, kifurushi cha kwanza cha COVAX zilizokataliwa au kutoa nusu ya chanzo zinazoundwa kwa mpango huo unaungwa mkono na WHO.

Mkurugenzi huyo alilalamikia ukosefu wa usawa kuhusu chanjo dhidi ya Covid-19 hali aliyosema imesababisha “mikondo miwili ya mkurupuko” ambapo mataifa ya Magharibi yamelindwa huku mataifa maskini yakiwa bado hatarini, akirelejea ombi lake la kuitisha msaada wa chanjo.

You can share this post!

Pasta asherehekea kufariki kwa nabii TB Joshua, asema...

Wabunge watisha kuvuruga usomaji bajeti Alhamisi