• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 12:48 PM
Wizi: Madereva wa matrela wanavyolazimika kulala mvunguni mwa lori kulinda mafuta      

Wizi: Madereva wa matrela wanavyolazimika kulala mvunguni mwa lori kulinda mafuta     

NA RICHARD MAOSI

MADEREVA wa matrela ya masafa marefu wanalazimika kulala mvunguni mwa lori ili kuyalinda mafuta dhidi ya wezi ‘wanaoyafyonza’ nyakati za usiku.

Vifaa vingine vya thamani ambavyo wezi hulenga ni pamoja na betri na mahema ya kufunikia mizigo, hasa muda huu wakati ambapo mvua ya El-Nino imeanza kushuhudiwa katika sehemu nyingi za nchi.

Kutokana na hali hii, baadhi ya madereva huendelea kuyaendesha malori wakiwa na usingizi au kwenye mvua kali kwa hofu ya kuibiwa.

Maeneo ambayo yamemulikwa kwa kuwahangaisha madereva ni Makindu, Kituo Cha Kibiashara cha Mlolongo, Maai Mahiu, Chimoi, Kaburengu, Kikopey na Salgaa.

Wanasema wamekuwa wakiibiwa mafuta pale wanapokuwa wamepakia malori kando ya barabara kupumzika baada ya kulemewa na uchovu wa safari ndefu.

Taifa Leo Dijitali ilizungumza na dereva Viggy Kimani, ambaye anasema hatasahau siku moja alipokuwa akisafiri kutoka Mombasa akielekea Kampala.

Alipofika eneo la Makindu alitafuta sehemu salama karibu na Mulika Mwizi, kisha akalala ndani ya gari lakini jua lilipochomoza, asubuhi alikuta tangi la mafuta likiwa wazi.

Anasema alikuwa ameibiwa zaidi ya lita 300 ambayo ilimgharimu Sh60, 000 na kuazia siku hiyo aliapa hawezi kusimama tena Makindu hata iwe ni mchana.

“Wezi walikuwa wamenyonya mafuta yote na ilibidi nimpigie mdosi simu. Hata ingawa alinitumia pesa za mafuta shingo upande, alinikata kwenye mshahara,” akasimulia dereva huyo.

Kimani anawaomba wamiliki wa magari kuwaongezea mafuta hususan wakati huu ambapo bei ya mafuta imepanda, kiasi kwamba mara nyingi hukatika njiani wakiendelea na safari.

Mwathiriwa mwingine ni Bw Kelvin Mkamburi, anayeorodhesha visa kadhaa lori analoendesha kufyonwa mafuta.

“Makindu, Mlolongo na Salgaa, nimeathirika kupata tangi halina chochote,” Mkamburi akaambia Taifa Leo Dijitali.

Aidha baadhi ya wezi hunyemelea hema za matrela hususan katika maeneo ya Salgaa au Sachangwan.

Mfano, Mkamburi anasema unapofika eneo la Maai Mahiu wezi hupigiana simu na wengine wao hupatiwa jukumu la kumfuata dereva kila aendapo huku kundi jingine likiendelea kuiba.

  • Tags

You can share this post!

Penzi la mauti: Mume katili alivyoangamiza mke kwa kumdunga...

Mbinu ya kijamii inayotumika Pokot Magharibi kuzima...

T L