• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Ziara 38 ndani ya mwaka mmoja!

Ziara 38 ndani ya mwaka mmoja!

Na CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto ameendeleza mtindo wa mtangulizi wake, Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta wa kufanya ziara nyingi katika nchi za nje, zinazogharimu mamilioni ya fedha Wakenya wakizongwa na mzigo wa gharama ya maisha na ushuru wa juu.

Ziara yake ya sasa nchini Saudi Arabia ni ya 38 ndani ya mwaka mmoja tangu alipoingia mamlakani mnamo Septemba 13, 2022; idadi inayozidi ziara zilizofanywa na watangulizi wake katika kipindi sawa na hicho.

Kwa mfano, uchunguzi wetu umeonyesha kuwa, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alifanya ziara 13 za nje katika mwaka wake wa kwanza afisini, kati ya Machi 2013 hadi Machi 2014. Ziara hizo ziligharimu mlipa ushuru Sh1.56 bilioni.

Naye Hayati Mwai Kibaki alifanya jumla ya ziara 33 pekee katika mataifa ya kigeni katika kipindi cha miaka 10 aliyoongoza Kenya kama Rais.

Kulingana na mtandao wa Wikipedia, Rais Ruto alifanya ziara 11 katika nchi za kigeni tangu alipoingia Ikulu Septemba 13, 2022 hadi Desemba mwaka huo.

Ziara yake ya kwanza ugenini ilikuwa nchini Uingereza mnamo Septemba 18, 2022, alipohudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II.
Aidha, kuanzia Januari mwaka huu hadi mwezi huu Dkt Ruto amefanya ziara 27 katika mataifa ya nje, huku akitembelea nchi zingine zaidi ya mara moja.

Ziara ya hivi punde ni ya Oktoba 14 aliyoifanya nchini China, kwa siku nne, kuhudhuria Mkutano wa Tatu wa Kimataifa kuhusu Barabara na Miundo Msingi.

Hata hivyo, mtindo wa Rais Ruto wa kufanya ziara nje kila mara haziwafurahisha baadhi ya Wakenya ikizingatiwa kuwa hugharimu pesa nyingi za mlipa ushuru.

Hii ni kwa sababu, kwa kawaida kiongozi wa taifa huandamana na ujumbe mkubwa wa maafisa wa serikali, walinzi na wasaidizi wengine.

“Japo ziara hizi ni muhimu ikizingatiwa kuwa rais hufanya mazungumzo na viongozi wenzake kuhusu udumishaji na uimarishaji wa ushirikiano wa kimaendeleo kati ya nchini hizo na Kenya, zinafyonza fedha nyingi. Pesa hizo zinafaa kuelekezwa katika shughuli zingine za maendeleo na rais afanye mikutano kama hiyo kwa njia ya mtandao,” alisema mchanganuzi wa masuala ya uongozi, Barasa Nyukuri Juni mwaka huu.

Katika bajeti ya mwaka huu wa kifedha wa 2023/2024, Afisi ya Rais iliomba mgao wa Sh2 bilioni kufadhili ziara za nje za Dkt Ruto kuanzia Julai 1, hadi June 30, 2024.

Hata hivyo, Wizara ya Fedha ilitenga Sh700 milioni kwa ziara hizo, pesa ambazo huenda zikaongezwa katika bajeti ya ziada itakayowasilishwa bungeni hivi karibuni.

Mtindo wa Rais Ruto, na hata naibu wake Rigathi Gachagua wa kusafiri katika nchi za kigeni unaenda kinyume na mpango wa serikali yake wa kupunguza ziara za maafisa wakuu. Bw Gachagua kwa sasa pia yuko ziarani katika nchi za Ubelgiji na Ujerumani.

Mnamo Novemba 22, serikali, kupitia Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u, ilidhibiti idadi ya ziara ambazo maafisa wake wanaweza kufanya katika mataifa ya ng’ambo.

Isitoshe, mapema mwezi huu, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei alitoa tangazo sawa na hili akisema hatua hiyo inalenga “kupunguza ubadhirifu wa pesa za umma”.

Lakini Rais Ruto amewahi kutetea ziara zake za kila mara katika nchi za kigeni akisema, ni sehemu ya mpango wake kustawisha uchumi na kuzalisha nafasi za ajira.

“Tunahitaji nafasi milioni moja za ajira ambazo niliwaahidi Wakenya. Hii ndio maana mimi huzuru nchi kama vile Amerika, Canada, Ufaransa na nchi za Kiarabu kutia saini mikataba na wawekezaji ili waje Kenya kuanzisha miradi ya maendeleo,” akaeleza alipohudhuria hafla ya kusherehekea uteuzi wa Chris Kiptoo kuwa Katibu wa Wizara ya Fedha, katika kijiji cha Kapteren, Keiyo Kaskazini, kaunti ya Elgeyo Marakwet.

  • Tags

You can share this post!

PK Salasya alia baada ya ‘kulemewa’ na bei ya viatu...

Arati apiga abautani kuhusu tozo za kesha, mikutano ya...

T L