Habari Mseto

#10YearChallenge: Ithibati ya uchumi kuimarika na teknolojia kukua

January 17th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

WATUMIZI wa mitandao ya kijamii nchini wamekuwa wakiendesha kampeni ambayo imepata umaarufu siku mbili zilizopita, ambapo wanachapisha picha zao za sasa na za miaka kumi iliyopita kuonyesha tofauti.

Na kilichobainika kutokana na picha hizo ni kuwa maisha ya watu wengi yameimarika kiuchumi kwa sasa ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita, yote kutokana na subira na bidii maishani.

Shindano hilo kwenye mitandao ya Twitter na Facebook, kwa jina #10yearchallenge limewavutia watu wa matabaka mbalimbali, pamoja na mashirika na kampuni tofauti, wote wakisherehekea kupita kwa mwongo.

Walichohitajika kufanya watumizi ni kuchapisha picha yam waka 2009 pamoja na nyingine ya 2019, kisha marafiki na umma kwa jumla unajionea tofauti na kufurahia.

Baadhi ya picha, hata hivyo zimeibua ucheshi, zingine zikionyesha namna baadhi ya watu walikuwa katika hali tofauti kabisa miaka kumi iliyopita, aidha kimwili, kifedha ama hata kimazingira.

Shindano lenyewe lilianza Jumatatu na kuendelea kutawala mitandaoni Jumanne, huku kampuni tajika ka Nation Media Group (kupitia NTV na Daily Nation), pamoja na wasanii tajika wakishiriki na kuleta burudani mitandaoni.

Baadhi ya picha ambazo watumizi wa mitandao walifurahia ni zile zilizoonyesha watu wakiwa na rangi nyeusi zaidi ikilinganishwa na sasa.

Zoezi hilo pia liliashiria jinsi teknolojia imekua, hasa kamera za simu zilizoimarika sana kwa ubora, na kuweza kutoa picha halisi ya mtu.