Makala

MOSES DOLA: Mwanahabari ndani mwongo mzima kwa mauaji

November 30th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

NDOTO na matumaini ya mwanahabari  Moses Dola Otieno,  kusherehekea Krismasi na Mwaka Mpya na familia yake yaliambulia patupu Alhamisi aliposukumwa jela mwongo mmoja.

Baada ya kuhukumiwa na Jaji Roselyn Korir, mwanahabari huyo alisimama kwa muda wa dakika tano akitazama dari la mahakama hata ikabidi afisa aliyemtia pingu kumgusa akimweleza aketi.

Dola alikaa kwa muda wa dakika 15 huku dada yake akimtazama.

Alipotoka nje ya mahakama aliliwaambia wanahabari, “Niacheni niende kuanza kutumikia kifungo.”

Mahabusu huyo aliinua mikono na kuwaaga dada na mama yake huku ameinua mikono ishara ya kushindwa na kusema “Hewala. Yamekuwa jinsi sikutarajia.”

Moses Dola atiwa pingu baada ya kuhukumiwa. Picha/ Richard Munguti

Akizugumza na Taifa Leo Djitali, Dola alikuwa na matumaini kwamba atapewa kifungo cha nje.

“Ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia imesema nifungwe nje,” Dola alimweleza dada yake wakizugumza kizimbani.

“Leo mkanitayarishie kitoweo cha kuku kwa vile nitafungwa nje,” alisema Dola.

“Hata sio kuku mmoja, watakuwa kadhaa,” alisema dada yake akimjibu.

Matamshi hayo yaliwapa matumaini dada yake lakini walikufa moyo pamoja naye kisha wakamhimiza wakimweleza , “Mungu yuko pamoja nawe.”

Wakati wa kusomwa kwa hukumu hiyo , watu wa familia ya Wambui hawakufika kortini.

Jaji Korir alisema taarifa ya familia ya mhasiriwa imeonyesha bado inaumwa na kuuawa kwa binti yao na kusema “adhabu nzuri ni kifungo cha gerezani.” Picha/ Richard Munguti

Wazazi na nduguze Wamboi walipohojiwa na afisa wa urekebishaji tabia walisema, “Kifo cha Wambui kilituuma sana.Tutaishi na kovu la kuuawa kwake milele. Hatujamsamehe mshtakiwa.”

Familia hiyo iliomba korti itekeleze sheria jinsi ilivyo ikimwadhibu mkwe wao.

Dola alisukumiwa kifungo hicho na Jaji Roselyn Korir aliyempata na hatia ya kuua bila kukusudia miaka saba iliyopita katika mtaa wa Umoja mnamo Mei 1, 2011.

Baada ya kumuua mkewe , Dola , alijisalamisha kwa polisi katika kituo cha polisi cha Naivasha kisha akarudishwa kituo cha Buruburu.

Akipitisha hukumu, Jaji Korir , alisema Dola alimuua mkewe kwa sababu ya matatizo aliyokuwa ameyapata kwa kupoteza kazi.

“Endapo kila mtu aliyepoteza kazi atakuwa akiua mkewe ama mpenziwe ni vifo vigapi vitatekelezwa humu nchini ikitiliwa maanani idadi kubwa ya watu waliopoteza kazi?” Dola aliulizwa na jaji. Picha/ Richard Munguti

Jaji huyo alisema lazima kila mtu ajifunze kuvumilia pasi kuchukua sheria mikononi.

“Hii korti itakuwa inakosea kutomwadhibu mshtakiwa kwa kosa la kumwangamiza  mkewe bila sababu,” alisema Jaji Korir.

Alisema ijapokuwa Dola hakukusudia kumuua mkewe, aliyakatiza maisha ya mkewe ambaye watu wa familia yake  walikuwa na matumaini makubwa naye.

Kufikia kifo cha Wambui alikuwa ripota na mtangazaji wa kituo cha televisheni cha NTV.

Jaji Korir alisema mshtakiwa aliomba asihukumiwe kifungo cha gerezani bali afungwe nje kusudi amlee mwanawe.

Wakili Cliff Ombeta aliyemwakilisha Dola aliomba mahakama impe mashtakiwa fursa ya kujirekebisha na kurejeana na wakwe zake.

Jaji Korir alisema kesi dhidi ya Dola ni mojawapo ya kesi ambapo familia na mshtakiwa na familia ya marehemu ziliomba zipewe nafasi ziridhiane.

“Tangu mshtakiwa apatikane na hatia ya kuua familia yake haikuchukua hatua ya kufanya mashauri ya maridhiano. Itakuwa ni ukiukaji wa sheria kutomwadhibu Dola,” alisema Jaji Korir.

Jaji huyo alisema lazima sheria ifuate mkondo na kumwadhibu mshtakiwa kwa mujibu wa sheria.

Jaji alisema ijapokuwa Bw Ombeta na Dola mwenyewe waliomba korti iwe na huruma ikipitisha hukumu ukweli uliopo ni kwamba mwanaye  Dola “ atakosa mapenzi ya mama kutokana na kitendo cha hasira cha mshtakiwa.”

Akijitetea, Dola alimweleza jaji kuwa kifo cha mkewe kilimwathiri pakubwa maishani. Picha/ Richard Munguti

Akasema Jaji Korir, “Maisha ya Wamboi yalikatizwa na mwanawe kupokonywa mapenzi ya mama. Kitendo cha mshtakiwa kilisababisha haya na lazima aadhhibiwe kwa mujibu wa sheria.”

Pia aliomba mahakama izingatie kuwa tangu akamatwe hakupata fursa ya kwenda kumtembelea mwanawe.

“ Naomba mahakama inipe fursa ya kumlea mwanangu. Nimezugumza naye kwa njia ya simu,” Dola alimweleza jaji.

Kiongozi wa mashtaka Catherine Mwaniki aliomba mshtakiwa asukumiwe kifungo cha jela na wala asihukumiwe kifungo cha nje.

Bi Mwaniki alisema licha ya mshtakiwa kuwasilisha tetezi hizo zote “ korti haitamuhukumu nje.”

Mahakama ilisema kuwa mshtakiwa atasilia korokoroni kwa muda wa miaka 10 na kumpa fursa ya kukata rufaa katika muda wa siku 14.