Habari Mseto

14 waliotangamana na aliyeugua corona watupwa kwa karantini

June 15th, 2020 1 min read

NA ELIZABETH OJINA

WATU wasiopungua 14 waliotangamana na mgonjwa wa corona kaunti ya Nyamira Jumapili wametafutwa na kuwekwa karantini.

Kisa hicho ni cha mwanaume wa miaka 46 kutoka Kebiringo aliyeingia Nyamira kutoka Nairobi.

Maafisa wa afya wa kaunti walimchukua na kumweka karantini katika kituo cha karantini cha shule ya wasichana ya Sironga.

“Kwa bahati mbaya sampuli zilizopelekwa kwenye kituo cha utafiti Kisumu Juni 12, 2020 zilipatikana kuwa ana virusi vya corona,” alisema Gavana John Nyagarama.

Baada ya kupokea majibu hayo, maafisa wa kushughulikia dharura walimpeleka katika hospitali ya rufaa ya Nyamira ambapo amelazwa.

Visa hivyo vilikuwa kati ya visa 137 vilivotangazwa Jumapili.

“Waliotangamana na mgonjwa huyo wanaendelea kutafutwa ili kuhakikisha kuwa wamewekwa kwenye karantini. Hao 14 wamewekwa karantini katika kituo cha masomo na udaktari cha Nyamira,’’ alisema Bw Nyagarama .