Makala

‘Daudi’ Omtatah anayetutumuana na ‘magoliathi’ serikalini

January 6th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KWA kawaida, hotuba ya Rais mara nyingi hurejelea masuala ya kitaifa na sera ambazo serikali yake imeweka ili kuboresha maisha ya Wakenya.

Huo ndio umekuwa mtindo ambao umekuwepo nchini, tangu enzi ya marais Jomo Kenyatta, Daniel Moi, Mwai Kibaki, Uhuru Kenyatta na sasa, Dkt Willim Ruto.

Ikiwa hotuba ya Rais itamrejelea mtu binafsi—ambalo ni tukio nadra sana—mara nyingi mtu huyo huwa ameiletea sifa nchi, au amefanya kitendo cha kipekee.

Hata hivyo, hali ni kinyume kwa Seneta Okiya Omtatah wa Busia, ambaye amegeuka kuwa gumzo kwa serikali ya Kenya Kwanza, yake Rais Ruto.

Kwenye Hotuba ya Mwisho wa Mwaka kwa Wakenya kutoka Ikulu ya Nakuru, Jumapili wiki iliyopita, Rais Ruto alimtaja Bw Omtata kuwa “mmoja wa vizingiti vikuu kwenye juhudi za serikali ya Kenya Kwanza kutimiza miradi yake”.

Rais Ruto alilalamikia hatua ya Bw Omtata kuwasilisha kesi mahakamani kupinga mpango wa serikali kuwatoza wafanyakazi ada ya makato ya nyumba.

“Ni kinaya wakati afisa wa serikali anapofika mahakamani kupinga mpango wa kuwajengea nyumba mamilioni ya raia, ilhali yeye amepewa mkopo wa nyumba wa riba ya chini na serikali anayoishtaki,” akasema Rais Ruto, bila kumtaja Bw Omtata moja kwa moja.

Mnamo Mei mwaka uliopita, Rais Ruto alimrai Bw Omtata hadharani kutofika mahakamani ili kupinga mpango huo.

Rais Ruto alitoa kauli hiyo kwenye ziara aliyokuwa amefanya katika Kaunti ya Busia.

“Bw [Omtata], unataka kunipeleka mahakamani na kile ninachofanya ni kubuni ajira kwa hawa watu? Hutaki wafaidike kwa maelfu ya ajira zitakazopatikana? Wakazi wa Busia, tafadhali mwambieni mtu huyu asitupeleke mbio sana,” akasema Rais Ruto.

Hata hivyo, Bw Omtata alimjibu kwamba alikuwa ashayarisha orodha ya malalamishi ambayo angewasilisha mahakamani, hivyo hangerudi nyuma.

Kulingana na wadadisi, kauli ya moja kwa moja ya Rais Ruto kwa Bw Omtata inaonyesha kuwa si mtu anayechukuliwa vivi hivi tu.

Wanasema kuwa ikizingatiwa Bw Omtata amekuwa kama mtetezi wa raia mahakamani kwa muda mrefu, Rais Ruto anafahamu kwamba juhudi zozote za serikali kumzima au kumyamazisha zitaonekana kama tishio dhidi ya “sauti ya raia”.

“Ikumbukwe kwamba Bw Omtata hajaanza harakati za kuwatetea raia wakati huu. Alianza wakati wa serikali ya Bw Kibaki. Aliendeleza harakati zake wakati wa utawala wa Bw Kenyatta. Ameshinda kesi kadhaa dhidi ya serikali za hapo awali, jambo ambalo limemzolea umaarufu mkubwa miongoni mwa Wakenya kutoka sehemu tofauti,” asema Bw Mark Bichachi, ambaye ni mdadisi wa masuala ya utawala.

Anasema kuwa umaarufu aliopata ndio ulichangia pakubwa yeye kuchaguliwa kama Seneta wa Busia mnamo 2022 kwa tiketi ya ODM.

“Licha ya kuchaguliwa kwa tiketi ya ODM, Bw Omtata ameibukia kuwa kipenzi cha wengi, bila kujali miegemeo yao ya kisiasa,” akasema Bw Bichachi.