Habari

Sarafu mpya bila nyuso za marais

December 12th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

BENKI Kuu ya Kenya (CBK) Jumanne ilizindua sarafu mpya ambazo zinawiana na viwango vinavyohitajika kikatiba huku picha za marais wa awali zikiondolewa.

Sarafu ambazo zitatumika sasa zina picha za wanyama pori pamoja na ishara nyingine za utaifa na kulinda utamaduni wa Kenya.

Hii ni mara ya kwanza kwa sarafu za aina hiyo kutengenezwa nchini tangu uhuru. Hilo ni mojawapo ya mapendekezo ya katiba ya 2010 ambayo bado hayakuwa yametekelezwa.

Sarafu ya Sh5 ina picha ya Kifaru, ya Sh10 picha ya simba na ya Sh20 picha ya ndovu. Upande wa pili wa sarafu hizo zote una picha za simba wawili kwenye mchoro ulioandikwa ‘Harambee’ chini yake, ishara ambayo imekuwepo hata katika sarafu za zamani.

Akiongoza uzinduzi wa sarafu hizo, Rais Uhuru Kenyatta alisema zinaashiria mwanzo mpya wa taifa katika hali ya kuijenga na kuhifadhi historia yake.

“Serikali yangu imeshuhudia kubadilishwa kwa sarafu za kisasa kulingana na katiba mpya. Sarafu hizi zina uwezo wa kuwasaidia hata watu wenye matatizo ya macho, ambalo ni jambo la kupongezwa,” akasema Rais Kenyatta.

“Sarafu mpya ni njia ya kujijenga, kuhifadhi historia na utamaduni na kulinda mazingira yetu. Zinaakisi mambo makuu ambayo ni yenye umuhimu kwa taifa,” Rais alisema.

Gavana wa Benki Kuu Dkt Patrick Njoroge alisema benki hiyo inapanga kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa picha na muundo wa sarafu mpya, akisema walizingatia maoni ya umma kabla ya kuamua muundo utakaotumiwa.

“Sarafu mpya zinawiana na matakwa ya katiba ya 2010 ki muundo na ishara. CBK ilialika umma kutoa maoni yake kuhusu muundo wanaotaka na ikachagua ule bora zaidi kulingana na mahitaji ya kiufundi na ambao unaakisi malengo ya taifa na kufuata mahitaji ya kikatiba,” akasema Dkt Njoroge.

Alisema sarafu hizo zilitolewa kwa mara ya kwanza Desemba 11, akisema zitafaa katika kuelimisha watu, kuhifadhi utamaduni na kuendeleza upekee wa Kenya duniani.

Waziri wa Fedha Henry Rotich ambaye alikuwepo alipongeza hatua hiyo ya Benki Kuu, akisema itafaa taifa kiuchumi.

Wakati huo huo Rais Kenyatta na Dkt Njoroge walitoa mwito kwa wakuu wa benki za humu nchini ambao walikuwa wamehudhuria hafla hiyo kutilia maanani suala la kuwapa mikopo wafanyabiashara wadogo wadogo (SMEs) na vijana, ili kusisimua uchumi.

Rais Kenyatta alisema kuwa benki zimekuwa zikikosa kuwafadhili wafanyabiashara hao ambao ndio wanaendesha uchumi wa taifa, zikipendelea tu kutoa mikopo kwa kampuni kubwa kubwa na serikali, kwa kudhani kuwa wafanyabiashara hawawezi kulipa.

“Kuna wafanyabiashara wengi ambao watasaidika na mikopo ya benki lakini bado sekta hii haijawafaa ipasavyo. Hawa ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu kwani tukiwainua watasaidia kuunda nafasi zaidi za kazi,” Rais akasema.

Alisema kuwa, vijana vilevile wana mipango mizuri na mawazo ya kibiashara lakini hawana pesa za kuanzisha, akizitaka benki kuwasikiza na kuwapiga jeki, bila ya kuwanyima mikopo kwa kuwa hawana dhamana ya mikopo hiyo.

Rais Kenyatta aliahidi kuwa serikali yake iko tayari kushirikiana na benki na kuzipa mkono wa msaada ili kuinua biashara hizo, akizitaka kuchukua hatua mwafaka kuanzia mwaka  2019.