Jamvi La Siasa

Pesa, madai ya usaliti yanavyochongea ukuruba wa magavana na maseneta kuyeyuka

February 5th, 2024 2 min read

NA WAANDISHI WETU

UKURUBA mkubwa wa kisiasa uliokuwepo baina ya magavana na maeneta wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2022 katika baadhi ya kaunti, sasa umevurugika na kugeuka mirengo pinzani ya kisiasa.

Wengi wao walichaguliwa kwa miungano sawa ya kisiasa na wengine katika mirengo tofauti.

Baadhi ya masuala yanayotajwa kuzua migawanyiko hiyo ni vita vya udhibiti wa mabilioni ya pesa yanayotolewa kwa kaunti, kutozingatiwa kwa mikataba ya kisiasa, michakato ya utoaji zabuni na nia za baadhi ya wanasiasa kuinua nyota zao kisiasa.

Baadhi ya kaunti ambazo zimejipata kwenye mivutano hiyo ni Nakuru, Meru, Narok, Kitui, Bomet, Machakos, Uasin Gishu, Kiambu, Kakamega na Nandi.

Magavana katika kaunti hizo wamekuwa wakiwalaumu maseneta dhidi ya kutumia nafasi zao kuwahangaisha na kujiongezea umaarufu kisiasa, wanapojitayarisha kwa uchaguzi mkuu ujao.

Katika Kaunti ya Narok, Gavana Stepgen Ole Ntutu na Seneta Ledama Ole Kina wamekuwa wakizozana kuhusu uendeshaji wa miradi ya maendeleo na usimamizi wa fedha zinazotokana na ada zinazokusanywa kutoka Mbuga ya Wanyama ya Maasai Mara.

Mizozo hiyo iko kwenye sekta za afya, barabara na utaii. Bw Ledama amekuwa akiikosoa serikali ya Bw Ntutu dhidi ya utumizi mbaya fedha hizo. Pia, amekuwa akiilaumu serikali hiyo dhidi ya kutowajibikia Sh451 milioni zinazotokana na makusanyo ya ada zinazolipwa na watalii katika mbuga hiyo.

“Barabara kadhaa, hospitali na chekechea (ECDEs) ziliachwa bila kukamilishwa na wanakandarasi, hata baada ya serikali ya kaunti kuwalipa fedha. Kinaya ni kuwa, hakuna hatua zozote ambazo zimekuwa zikichukuliwa wanakanadarasi hiyo, kwani wananchi hawajakuwa wakifaidika na miradi hiyo,” akasema.

Katika Kaunti ya Bomet, Gavana Hillary Barchok amekuwa kwenye mvutano na Seneta Hillary Sigei. Ni mvutano ambao uwawagawanya madiwani katika kaunti hiyo.

Prof Barchok amekuwa akidai kwamba Bw Sigei amekuwa akiipaka tope serikali kwa kisingizio cha kufuatilia utendakazi wake.

Hata hivyo, Bw Sigei amekuwa akipuuza madai hayo.

Katika Kaunti ya Meru, juhudi za kumng’oa mamlakani Gavana Kawira Mwangaza zimeibua mivutano mikali ya kisiasa katika kaunti hiyo. Juhudi hizo zimekuwa zikiungwa mkono na Seneta Kathuri Mirungi.

Bi Mwangaza amekuwa akimlaumu Seneta huyo kwa kushirikiana na naibu wake, Isaac Mutuma, na Waziri wa Kilimo Mithika Linturi kuendesha njama hizo.

Katika Kaunti ya Kakamega, Seneta Boni Khalwale ameshirikiana na aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo, Wycliffe Oparanya, kuukosoa uongozi wa Gavana Fernandes Barasa.

Wawili hao wanamlamu Barasa kuwa kukosa kutoa basari za kutosha kwa wadi.

Katika Kaunti ya Nakuru, Gavana Susan Kihika wamekuwa wakikabiliana vikali na Seneta Tabitha Karanja kutokana na utata unaohusu umiliki wa ardhi ilikojengwa Nakuru War Memorial Hospital.

Wawili hao walichaguliwa kwa tiketi ya UDA. Bi Karanja ametishia kuwashinikiza madiwani kumng’oa mamlakani Bi Kihika.

Katika Kaunti ya Nairobi, Seneta Edwin Sifuna amekuwa akimlaumu Gavana Johnson Sakaja kwa ufisadi.

Katika Kaunti ya Nandi, Seneta Samson Cherargei amekuwa akimlaumu Gavana Stephen Sang’ kwa kutoa zabuni kwa washirika wake pekee.