Michezo

15 wasonga mbele Shield Cup, Ulinzi na Sofapaka zang’olewa

March 19th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU 15 zilijikatia tiketi ya kushiriki mechi za raundi ya 16-bora za kipute cha SportPesa Shield, ambacho mshindi huingia Kombe la Mashirikisho la Afrika.

Mabingwa watetezi Kariobangi Sharks pamoja na Western Stima, Congo Boys, SS Assad, Bungoma Superstars, Murang’a Seal, Bidco United, Dero, KCB, Vihiga Sportif, Kariobangi Sharks, AFC Leopards na Bandari, zilifuzu Jumamosi.

Nazo Wazito, Mwatate United na Equity zilijikatia tiketi Jumapili.

Klabu mbili kati ya nane kutoka Ligi Kuu ya KPL zilizoingia katika mashindano haya msimu huu zilibanduliwa nje mapema.

Klabu hizo ni pamoja na Sofapaka na Ulinzi Stars.

Zote zililemewa katika upigaji wa penalti dhidi ya Bungoma Superstars na SS Assad mtawalia.

Gor Mahia vs Kenpoly

Nafasi ya mwisho iliyosalia itajazwa Jumatano baada ya washikilizi wa rekodi ya mataji mengi katika mashindano haya, Gor Mahia (10), watajibwaga uwanjani MISC Kasarani kupepetana na limbukeni Kenpoly.

Klabu hizi zilikutana mnamo Juni 20, 2018, katika hatua hii ya 32-bora na Gor ikatamba kwa kufunga mabao 5-0.

Gor Mahia ambayo itaanza mchuano huo na motisha kubwa kutokana na ufanisi wa kuingia robo-fainali ya Kombe la Mashirikisho baada ya kuzima Petro de Luanda kutoka Angola jijini Nairobi siku ya Jumapili, ililemewa na Sharks katika robo-fainali ya SportPesa Shield mwaka 2018.

 

Matokeo ya mechi za raundi ya 32-bora:

Uprising 0-5 Western Stima, Congo Boys 2(3)-2(2) Kenya Police, SS Assad 0(5)-0(4) Ulinzi Stars, Bungoma Superstars 0(5)-0(4) Sofapaka, Murang’a Seal 4-1 Kisumu All Stars, Transmara Sugar 0-1 Bidco United, Dero 2-0 FC Talanta, Sindo United 0-1 KCB, Vihiga Sportif 2-0 Ushuru, Elim 0-5 Kariobangi Sharks, Transfoc 0-4 AFC Leopards, Kayo 0-1 Bandari, Fortune Sacco 0-1 Wazito, Emmausians 0-6 Mwatate United, Naivas 0-1 Equity.