Habari

COVID-19: Visa 15 zaidi vyathibitishwa nchini idadi jumla ikifika 715

May 12th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WATU wengine 15 wamepatikana na virusi vya corona nchini Kenya kipindi cha saa 24 zilizopita na kufikisha idadi ya maambukizi nchini kuwa 715.

Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman amesema Jumanne visa hivyo vilipatikana baada ya sampuli 978 kupimwa.

“Wakenya 14 ilhali mmoja ni raia wa Rwanda. Mwathiriwa mwenye umri mdogo zaidi ni mtoto wa umri wa mwaka mmoja,” amesema Dkt Aman.

Wagonjwa hao wapya wanatoka kaunti sita nchini. Watu saba wanatoka Mombasa, Migori (3), Wajir (2), Machakos (1), Kiambu (1), Wajir (1) huku Nairobi ikiandikisha kisa kimoja kipya.

Wagonjwa wapya kutoka Kaunti ya Mombasa wametoka katika maeneobunge ya Mvita (5), Jomvu (1), Kisauni (1) huku visa vya Migori vikipatikana katika maeneo ya Kuria Mashariki, Tebesi na Nyamarama.

Watu wawili waliopatikana na virusi vya corona katika Kaunti ya Wajir walikuwa wametangamana na wagonjwa wa kwanza ambao walikuwa wamesafiri kutoka Somalia.

Mgonjwa mpya wa Nairobi anatoka mtaa wa Githurai 44 huku yule wa Machakos akiwa mkazi wa eneobunge la Kathiani.

Dkt Aman amesema kuwa watu wanane zaidi walipona na kuruhusiwa kwenda nyumbani, na kufikisha 259 idadi ya waliopona kutokana na Covid-19 kufikia sasa.

“Na kwa bahati mbaya watu wengine watatu wamefariki na hivyo jumla ya watu ambao wamefariki ni 36,” amesikitika waziri huyo msaidizi.