Bambika

Njambi Koikai alikuwa na ‘vibe’ ya kipekee; wapenzi wa reggae watamkosa

June 7th, 2024 4 min read

“Aaah…. Dunia. Bado ni kiza, bado ni kiza na marashi ya dunia siyaskii,

Najihisi nipo kuzimu naishangaa sayari hii, iliyojaa wanasiasa, michezo na wasanii,

Najiuliza wamekuja huku kutalii au wameshajamia dunia ndo haijirudii…”

“Yee iye ite eeh. Dunia mapito jamaa tuwaombeeni waliokufa waende salama,

Mi nawe tupo hatujui siku yetu lini, kinachotakiwa tuishi kwa amani duniani.”

Sina uhakika kama mwendazake, mburudishaji maarufu Njambi Koikai almaarufu Fyah Mummah Jahmby aliwahi kuisikia rekodi hiyo, yake Matonya enzi za uhai wake.

Ila nilicho na uhakika nacho ni kwamba Fyah Mummah katika enzi za maisha yake ya utu uzima hata alipokuwa akihangaishwa na maradhi hatari ya Endometriosis, alipambania sana suala la vijana kuishi kwa amani duniani.

Alipambania sana kutaka kuona vijana wakipata nafasi za riziki na kwa nguvu hizo hizo alijitahidi kupambana na kuhamasisha kuhusu maradhi ya Endometriosis.

Jahmby kwa mara ya mwisho alivuta pumzi wiki hii na kuondoka duniani akiwa na umri wa miaka 38 siku mbili baada ya kuomba msaada wa damu ili kuendelea kupambania maisha yake dhidi ya Endometriosis. Kifo chake kimewaacha wengi wafuasi wake na huzuni mkubwa.

Nduru ilivyootesha nyota yake Fyah Mummah

Mtu wa kwanza kumpa kazi au ajira Fyah Mummah alikuwa ni mwanahabari aliyegeuka na kuwa mwanasiasa Sabina Chege.

Mojawepo ya sababu zilizochangia Bi Chege kumchora Njambi kazi ni nduru. Eeeh nduru. Hivyo ndivyo Njambi alivyoishia kupata ajira yake ya kwanza kama mtangazaji wa redio.

Kipindi hicho akiwa ni binti mdogo tu alikuwa amemaliza masomo yake ya chuo na kama ilivyo ada akapata fursa kama mwanagenzi kwenye shirika la kitaifa la habari KBC.

Njambi alikuwa kwenye studio za Metro FM alfajiri hiyo akiwa anasoma namna ya kuseti mitambo kutoka kwa mtangazaji na mwanahabari mkongwe Billy Odidi.

Wakati wakiwa wanaseti mitambo na kuitoa kutu, Odidi pia alikuwa anasubiri kufanya mahojiano na staa wa reggae aliyekuwa akitamba enzi hizo Sheldon Campbell almaarufu Turbulence.

Turbulence alipoingia studioni, wakati wakiwa hewani, Njambi alishindwa kuvumilia mshtuko wake wa furaha ya kumwona nyota anayemhusudu na kujikuta akiachia unyende wa kutishia.

“Nani huyo anapiga nduru hewani,” bosi Bi Chege aliyekuwa akifuatilia kipindi kutoka afisini mwake, akauliza.

Kwenye mahojiano, Odidi anasema kabla ya siku hiyo Njambi alimfuata na kumwomba amruhusu apige picha na Turbulence atakapokuja studio.

“Nilimwambia kama kweli unamhusudu kiasi hicho, badala ya picha tu, mbona usije tupige shoo sote ili na wewe upate fursa ya kumuuliza maswali. Siku hiyo, Njambi alifika mapema sana studioni,” Odidi kafunguka kwenye mahoajino na safu hii.

Ile nduru iliwashangaza wengi sio tu bosi Sabina. Odidi anamkumbuka binti mpole ila ile nduru ilimfanya kushangaa kama kweli yule ndiye Njambi ambaye amekuwa akimfahamu kwa siku kadhaa. Turbulence naye alishtuka na kudhani pengine kuna ishu.

“Sote tulishtuka hata Turbulence pia na kudhani kuna tatizo. Shoo ilikuwa kali ila Njambi alishindwa kumuuliza maswali sababu ya kuzidiwa na furaha ya kukutana na mojawepo ya mastaa wa reggae aliokuwa anawahusudu,” Odidi anaongeza.

Kikao na Sabina Chege

Baada ya shoo, Njambi alipata ripoti anatakiwa kwenye afisi ya bosi, na hofu yake ikawa ni kwamba atatimuliwa na fursa yake ya kuanza kujinoa kuwa mwanahabari itapotea.

“Kumtimua halikuwa wazo lililonipita akilini maana kwa namna alivyoachia ule unyende, kuna kitu kilichonifurahisha kuhusu nduru ile,” Bi Sabina alifunguka kwenye mahojiano na Bambika.

Bi Sabina zama hizo alikuwa ndio bosi wa stesheni 18 za radio za KBC.

“Alipoingia afisini nilifurahishwa sana na ile vibe yake maana enzi zile hawakuwepo mabinti wengi watangazaji. Nilimuuliza ni lini anaweza kuanza kufanya kazi kama mtangazji mwenza wa Odidi na ndivyo nilivyomwajiri.”

Huu ukawa ndio mwanzo wa safari yake Njambi kama mtangazaji shupavu wa shoo za reggae radioni nchini kazi ambayo alifanya katika stesheni kadhaa nchini.

Umaarufu wake ulipozidi, Njambi alianza pia kufanya kazi kama MCee wa matamasha ya reggae na hafla zingine zilizohitaji mfawadhi. Sifa kubwa yake Njamby ilikuwa ni uwezo wake wa kuichangamsha hadhira.

“Njambi alikuwa na vibe fulani hivi ambayo ilionekana kuwashika sana mashabiki hasa wale wa kiume. Hivyo ndivyo safari yake ya kuwa MCee vile vile ilianza.

Shoo yake ya mwisho

Kati ya mashabiki wa kiume walioishia kumpenda sana Njambi kwa kazi yake ni mchezaji soka wa zamani Bramwel Karamoja ambaye huandaa mashindano ya soka za mashinani akichanganya na burudani.

Shoo ya mwisho ambayo alimwalika Njambi ilikuwa Machi 31, 2024 katika uwanja wa Kinoru, Meru.

“Aliniomba nimruhusu aje na bendi ya reggae maana alitaka kufanya kitu tofauti. Kwa kawaida alikuwa akipiga shoo zake na DJ ambaye angechagua nyimbo za reggae ambazo Njamby angetumbuiza ila safari hii alitaka kufanya hivyo kwa kutumbuiza na laivu bendi. Alipiga shoo ya zaidi ya saa moja,” Karamoja anakumbuka.

Kabla hajamaliza mwendo Jumatatu hii, Njambi alikuwa tayari ameanza mchakato wa kuandaa shoo bab’kubwa kusherehekea kutimiza miaka 20 kwenye tasnia na biashara ya muziki wa reggae.

Na kisha astaafu.Karamoja tayari alikuwa sehemu ya watu ambao wangehusika kumsaidia kwenye maandalizi. Shoo hiyo ilikuwa ifanyike Agosti mwaka huu.

“Ilikuwa iwe shoo yake ya mwisho kama mburudishaji lakini pia shoo ya kusherehekea kutimiza miaka 20 kwenye gemu,” Karamoja anasema.

Vita dhidi ya maradhi ya ‘Endometriosis’

Ni ugonjwa ulioanza kumtatiza toka akiwa tineja lakini kutokana na uchache wa wataalamu wa endometriosi nchini, ilikuwa vigumu kuelewa kilichokuwa kikimsibu.

Hata wazazi wake hawakuelewa. Njamby anakiri naye hakujua kilichokuwa kikimkuta kwani kila alipopata hedhi lazima ingekuja na uchungu wa kupitiliza.

Njamby aliwahi kusema ilichukua miaka 16 kuja kugunduliwa kuwa anaugua endometriosis. Wakati ugonjwa huo unagundulika ilikuwa tayari umechelewa na ugonjwa wake ukawa umemwathiri sana.

Ila hata baada ya kuchelewa, Njambi alipambana na ugonjwa huo ikiwemo kufanyiwa upasuaji Marekani uliomfanya kuishi hospitalini kwa zaidi ya mwaka mzima.

Hadi analala, imekuwa safari ya gharama kubwa kwani matibabu yaligharamu mamilioni ya pesa. Lakini pia imekuwa ni safari ya machungu kwani hata kimahusiano Njambi aliwahi kukiri kushindwa kuwa na mpenzi kutokana na uchungu wakati wa tendo.

Lakini kwa wengi waliofanikiwa kufanya kazi naye ikiwemo mwanahabari mahiri Larry Madowo aliyefanya kazi naye Nation Media, Njambi pamoja na yote aliyoyapitia, aliishi maisha yake kwa furaha kubwa sana.

“Fyah Mummah safiri salama, nenda mama tutaonana baadaye,” aliposti mmoja wa mashabiki wake.

Ripoti ya SINDA MATIKO