Habari Mseto

Aliyevuruga hafla ya waziri kupimwa akili

June 15th, 2024 2 min read

RICHARD MUNGUTI NA NDUBI MOTURI

MWANAHARAKATI aliyebambwa na polisi Alhamisi kwa kuvuruga hafla ya kupigwa picha ya Waziri wa Fedha Prof Njuguna Ndung’u kabla ya kusoma bajeti ya 2024/2025 ameambia mahakama ya Milimani Nairobi hatanyamaza hata akifungwa jela miaka 100.

Julius Kamau Kimani alizua vurugu mbele ya Hakimu Mkuu Bernard Ochoi na kumtaka hakimu asiwe mwoga akisema wajasiri ndio watakaofaulu.

“Sitanyamaza hadi uongozi bora utakaposhamiri. Nchi hii inaongozwa na waongo, watu wasiojali, watu wasio na utu hata! Hawana shughuli na yeyote hata Wakenya wakiangamia kwa shida na gharama ya juu ya maisha. Hata nikifungwa gerezani miaka 100, sitaogopa kusema ukweli,” Kimani aliambia korti.

Kesi itatajwa Juni 17, 2024, kwa maagizo zaidi.

Wakati huo huo, Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya umekosoa bajeti iliyopendekezwa na serikali ya Rais William Ruto ya Sh3.914 trilioni ukisema inalenga kukuza ufisadi na sio maendeleo ya kufaidi walipa ushuru.

Vinara wa muungano huo walisema ikipitishwa na kutekelezwa, itafanya biashara nyingi kufungwa na maelfu ya Wakenya kukosa ajira, jambo litakalofanya uchumi kudorora.

Upinzani ulidai kuna Sh1 trilioni za “ufisadi uliopangwa kwenye bajeti” katika makadirio ya bajeti yaliyosomwa na Waziri wa Hazina ya Kitaifa Njuguna Ndung’u Alhamisi.

Ufisadi uliopangwa kwenye bajeti, upinzani ulisema, uliwasilishwa kwa njia ya Sh23.6 bilioni za matumizi ya kawaida katika sekta zote.

Katika taarifa iliyosomwa na Kiongozi wa Wiper Democratic, Kalonzo Musyoka, muungano huo ulihoji pesa zilizotengewa Afisi ya Rais (Sh1.2 bilioni), Afisi ya Naibu Rais (Sh678 milioni) na Wizara za Ulinzi (Sh11 bilioni), Mashauri ya Nje (Sh1.4 bilioni), Hazina ya Taifa (Sh6 bilioni), Uchukuzi Sh1.3 bilioni na Vyama vya Ushirika (Sh2 bilioni).

“Zaidi ya hayo, Hazina ya Kitaifa ina Sh26 bilioni zaidi kwa jina la maendeleo. Idara ya Serikali ya Ugatuzi ina ongezeko la Sh bilioni 2.6 za matumizi ya maendeleo. Ikiwa utawala huu unaamini katika kufaulu kwa ugatuzi, basi fedha hizi zinafaa kuwa sehemu ya mgao wa Serikali za Kaunti,” ilisema taarifa ya muungano huo.

Kuhusiana na Ushuru wa Magari, upinzani umesema hatua zilizopendekezwa za ushuru zitaongeza gharama ya umiliki wa gari na kutatiza shughuli za uchukuzi.

“Ushuru mpya wa magari unaopendekeza ushuru wa asilimia 2.5 kwa thamani ya gari, kwa kiwango cha chini cha Sh5, 000 na kisichozidi Sh100, 000, ukipitishwa utapandisha gharama ya umiliki wa gari na kusababisha kuongezeka kwa gharama ya bima. Utaathiri sekta ya uchukuzi na hivyo kuongeza gharama ya maisha, ” akaongeza Bw Musyoka.