Habari za Kitaifa

Rais Ruto kupunguza washauri, mashirika ya serikali


KATIKA hatua ya kupunguza matumizi, Rais William Ruto ametangaza kwamba atapunguza idadi ya washauri wa serikali kwa nusu.

Uamuzi huu unalenga kuongeza ufanisi ndani ya utumishi wa umma na unapaswa kutekelezwa mara moja.

“Idadi ya washauri katika serikali itapunguzwa kwa asilimia 50 huku watumishi wa umma waliofikisha umri wa kustaafu kuondoka mara moja,” Rais Ruto alisema wakati wa hotuba yake kwa Taifa.

Kupunguza huku ni sehemu ya mkakati mpana zaidi wa Rais wa kuondoa matumizi yasiyo ya lazima ya serikali na kuboresha utoaji wa huduma.

Kando na kupunguza idadi ya washauri, Rais Ruto alizindua mpango wa kufuta mashirika 47 ya serikali ambayo yana kazi zinazofanana.

Alisema watumishi hao kutoka katika mashirika hayo watapatiwa kazi nyingine katika wizara na idara mbalimbali ndani ya serikali.

“Mashirika arobaini na saba yenye kazi zinazofanana yatavunjwa, na hivyo kusababisha kuondolewa kwa gharama zao za uendeshaji. Kazi zao zitaunganishwa katika wizara husika,” Ruto alieleza.

Hatua hii inalenga kuondoa gharama, kurahisisha utendakazi wa serikali, na kuimarisha uratibu ndani ya utumishi wa umma.