Kimataifa

16 wafariki katika mkanyagano siku ya kuadhimisha uhuru

June 28th, 2019 2 min read

Na AFP

WATU 16 walifariki kwa kukanyagwa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika uwanja wa kitaifa nchini Madagascar jijini Antananarivo wakati wa sherehe za kuadhiminisha siku ya uhuru wa nchi hiyo.

Miili wa wahasiriwa hao 16, wakiwemo watoto watatu, ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya HJRA jijini humo.

Kulingana na mashahidi katika hospitali hiyo, kisa hicho kilitokea mwendo wa saba adhuhuri Jumatano katika uwanja wa michezo wa Mahamasina.

Maelfu wa wananchi walikuwa wamekongamana hapo kutazama gwaride la kijeshi lililoandaliwa kuadhimisha siku hiyo ya kitaifa.

Baada ya gwaride hilo la wanajeshi, maafisa wa usalama walifungua malango kadha ya kuingia uwanja huo ili kuwaruhusu wananchi kuondoka. Watu walianza kuondoka taratibu, kulingana na walioshuhudia kisa hicho.

Lakini kwa ghafla polisi walifunga malango hayo na kuwazuia watu kuondoka, hali ambayo mashahidi walisema ilisababisha msongamano mkubwa uliopelekea watu kukanyagana.

“Wakati ambapo waandalizi walifungua lango, tulikuwa mbele katika foleni. Lakini kwa ghafla polisi walifunga lango na kusababisha msongamano,” akasema Jean Claude Etienne Rakkotoarimanana, 29, ambaye alijeruhiwa katika purukshani hizo.

“Zaidi ya hayo watu, walikimbia mbele yetu. Walitugonga, wengine wakatuvuta na kupiga ndipo baadhi yetu wakaanguka na kujeruhiwa,” akaongeza. Alisema baadhi yao pia walizirai katika patashika hizo.

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina, katika kikao na wanahabari akiandamana na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame, alituma risala zake za rambirambi kufuatia vita hivyo.

“Kulikuwa na watu wengi ambao hawakuweza kuingia katika uwanja huo wa michezo, hali ambayo ilisababisha shida,” akasema Rais huyo.

Rais Rajoelina alisema kuwa serikali italipa bili za hospitali za wale wote ambao walijeruhiwa.

Jana, Rais huyo alitembelea hospitali ambako mamia ya watu waliojeruhiwa walikuwa wakipokea matibabu.

Itakumbukwa kuwa mnamo Septemba, 2018 tukio sawa na hilo lilitokea katika uwanja huo wa michezo na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku wengine zaidi ya 30 wakijeruhiwa.

Watu walikanyagana wakati walikuwa waking’ang’ania kuingia uwanjani humo kutizama mechi ya kandanda kati ya timu ya Madagascar na Senegal.

Na kabla ya hapo, mnamo Juni 26, 2016, miaka mitatu kamili kabla ya kisa cha Jumatano, mlipuko wa bomu ulitokea katika uwanja huo wa michezo wa Mahamasina wakati wa tamasha ya muziki. Watu watatu waliuawa na wengine wengi wakajeruhiwa.