Habari Mseto

Kampuni zajitokeza kumsaidia Ruth Jemutai

January 31st, 2019 3 min read

Na FLORAH KOECH NA PETER MBURU

MWANAMKE kutoka kaunti ya Baringo ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Chuka na ambaye licha ya kufuzu kwa alama bora zaidi, (First class honors) amekuwa akiishi katika lindi la umaskini nyumbani kwao hatimaye anaweza kutabasamu.

Hii ni baada ya kampuni kadha za humu nchini kujitokeza kumsaidia, baada ya habari kuhusu matatizo yake kimaisha kuangaziwa.

Tangu Jumatano, Bi Ruth Jemutai Rono alieleza Taifa Leo kuwa baada ya habari kuhusu namna amekuwa akiishi maisha ya uchochole na kufanya vibarua ili kuwalea ndugu zake kuangaziwa, watu wengi sasa wamempigia simu wakitaka kumpa kazi na kusaidia familia yake.

“Hospitali ya Reale ya Eldoret imenipigia simu, waliokuwa wahadhiri wangu Chuka aidha wameniita kufunza somo la biashara katika shule ya upili ya Ndagani, huku wakinitafutia kazi. Pia kuna kampuni eneo la Utawala Nairobi ambayo imeniitia kazi ya Sh30,000 na kuahidi kunipa nyumba bure na kuwapa ndugu zangu nyumba ili wawe wakisomea shule ya msingi ya Utawala,” Bi Jemutai akaeleza Taifa Leo.

Alisema kuwa pia kampuni ya Giselle Foundation kaunti ya Kisumu imeeleza nia yake kumuajiri kama mfanyakazi wa kudumu, kulipia ndugu zake karo na kutafuta mtu wa kuwalea. Hii ni licha ya serikali ya kaunti ya Baringo kueleza nia ya kumfunza kazi.

“Ninashukuru sana kwa wale wamejitolea kunipa kazi. Bado sijafanya uamuzi lakini niko tayari kufanyia kazi kampuni ambayo itanilipakutokana na matatizo niliyo nayo nyumbani,” akasema.

Wakati alipofuzu kutoka Chuo Kikuu cha Chuka mnamo 2015 na shahada ya Economics and Statistics na kupata alama ya juu zaidi katika masomo ya shahada, Bi Jemutai hakudhani kuwa umasikini mkubwa wa nyumbani kwao ungemnyima raha ya kuvuna matunda ya bidii yake kimasomo.

Lakini kwa bahati mbaya, Bi Jemutai wa miaka 27 aliishia kijijini kwao akifanya kazi za vibarua kuwasaida ndugu zake wadogo, wakati wazazi wake walitengana.

Jemutai anatoka kijiji cha Lelbatai, eneo la Baringo ya Kati na alilelewa katika makazi ya kimasikini, japo akajikakamua kwa bidii kusoma. Alipata alama 364 katika mtihani wa kitaifa wa KCPE mnamo 2005 na akajiunga na shule ya upili ya wasichana ya Tabagon.

Matatizo yake hata hivyo yalianza wakati wazazi wake walishindwa kupata pesa zilizohitajika kumpeleka kidato cha kwanza.

“Mamangu aliweza kupata Sh11,000 kwa kujikaza baada ya kufanya vibarua na nikajiunga na kidato cha kwanza. Hata hivyo, baadaye hakuna pesa zingine zozote zilizolipwa hadi nilipomaliza kidato cha nne, kwani na deni la Zaidi ya Sh90,000,” Jemutai akasema.

“Muda wote nikiwa shule ya upili, nilikuwa nikitumwa nyumbani kwa ajili ya karo, lakini nilirudi bila pesa za kulipa,” akasema.

Alipotembelewa nyumbani kwao na Taifa Leo Jumanne, ilibainika kuwa Jemutai, ambaye ni kifungua mimba kwa familia ya watoto wanane ndiye mtafuta riziki nyumbani kwao na mlezi wa dada zake wawili ambao ni walemavu, wanaohitaji ulezi wakati wote.

Mamake alirejea nyumbani kwa wazazi wake miaka mitatu iliyopita kutokana na matatizo ya ndoa, naye baba ni ameadhirika na ulevi kupindukia. Hali hiyo imemwacha Jemutai kama mlezi wa pekee katika familia yake.

Alieleza Taifa Leo kuwa alipokuwa shule ya upili, alilazimika kutembea kilomita 20 kwenda shuleni.

“Nilivaa viatu pea moja tangu nilipoingia hadi kutoka shule ya upili. Kila wakati wa kufungua shule ulipofika ama kufukuzwa kwa ajili ya karo, nilikuwa nikitembea Zaidi ya kilomita 20 kupitia milima na mabonde kufikia ndoto yangu,” akasema.

“Ningetembea bila viatu mwendo mrefu kasha kuvivaa nilipokaribia shule ili visiishe,” akasema.

Na licha ya matatizo haya yote, bado aliweza kufuzu kwa alama A- katika mtihani wa KCSE.

Wakati wa zawadi kutolewa kwa waliofuzu, walimu walieleza kuhusu changamoto zake kulipa karo na kwa haraka akachangiwa Sh52000.

“Nilitumia pesa hizo kulipa deni la karo na deni lililosalia shule ikanilipia,” akasema.

Alipojiunga na chuo kikuu cha Chuka, ni wakazi wa nyumbani kwao waliochanga pesa za kumsomesha. Jemutai anasema kuwa wakati huu alikuwa ameanza kupata motisha maishani, kwani licha ya kuwa kwao walikuwa masikini, aliona kuwa ndoto yake ilikuwa ikielekea kutimia.

“Hapo mkopo wa masomo HELB ulinifaa sana kusoma bila matatizo kwa miaka mine ya chuoni na nikafuzu kwa alama First Class,” akasema.

Hata hivyo, alipomaliza chuo kikuu, alirejea nyumbani na kumpata mamake akiwa mgonjwa sana. Baada ya miaka mingi ya matatizo ya ndoa, madaktari walibaini kuwa alikuwa ameadhirika.

“Singeweza tena kumtafutia matibabu na kulea ndugu zangu na hivyo wajomba zangu wakamchukua,” akasema Jemutai.

Aliendelea kukaa nyumbani akiwashughulikia ndugu zake na kumsomesha dadake aliyejiunga na kidato cha kwanza, wote wakifanya vibarua ilia some.

Alipopata cheti mnamo 2016, aliamua kutafuta vibarua Jijini Nairobi ili aweze kupata kitu cha kusaoidia familia yake, alipokumbuka matatizo ya nyumbani.

Lakini baada ya miezi mitatu alipokea habari kuwa babake alifika nyumbani na kuteketeza nyumba, ambapo ndugu zake walijeruhiwa vibaya. Aliamua kurejea nyumbani.

“Nilikuwa nimeweka hazina ya Sh10,000 ambazo nilianza kutumia kujenga nyumba mbili za matope na kuwatafuta ndugu zangu ambao walikuwa wakiishi kwa majirani,” akasema.

Tangu wakati huo, ji=uhudi zake za kutafuta kazi ili aweze kukimu mahitaji ya ndugu zake hazijakuwa zikifanikiwa, jambo ambalo limefanya maisha yake kuwa magumu sana kila uchao.

“Nimelazimika kufanya kazi ya kuwalea ndugu zangu wawili wachanga ambao ni walemavu. Nategemea pesa za vibarua kupata kila kitu,” akasema Jemutai.

Alisema kuwa tangu mamake alipougua, amekuwa akifanya kazi ngumu ya kuwashughulikia ndugu zake, kwani walikuwa wakiteseka sana.

“Nimefanikiwa kimasomo lakini matatizo mengi ya nyumbani yananivuta nyuma na siwezi kufurahia matunda ya kazi yangu ngumu niliyoweka masomoni,” akajutia.