Habari Mseto

MKU yatia saini mkataba na mashirika mawili ya kiafya

February 19th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO
CHUO Kikuu cha Mount Kenya kimeingia mkataba wa maelewano na Shirika la Afya la Switchnet, pamoja na Finders Keepers kwa minajili ya kuboresha maswala ya afya.
Ni kwenye hafla iliyofanyika Jumatatu katika mojawapo ya afisi ya Seneti katika chuo hicho ambapo wakuu wa shirika hilo walitia saini makubaliano hayo.
Naibu chansela wa Chuo cha Mount Kenya Profesa Stanely Waudo, alisema hatua hiyo ni ya kipekee kwa sababu itashughulika na kesi au maswala ya afya yaliyo ya dharura.
“Baadhi ya maswala muhimu yatakayolengwa kwanza ni upasuaji wa watoto walio na ulemavu ambao wanahitaji  upasuaji  wa dharura,”alisema Prof Waudo.
Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya Profesa Stanley Waudo (wa pili kutoka kulia) akiongoza kutia saini mkataba na mashirika mawili ya huduma za kiafya kwa lengo la kuboresha maswla ya kiafya kupitia upasuaji na utafiti. Picha / Lawrence Ongaro
Miongoni mwa maswala mengine wanayolenga kufanya ni wanawake walio na matatizo ya kujifungua kwa kawaida na hivyo inawalazimu kujifungua kwa upasuaji wa haraka.
Pia watashughulikia wagonjwa ambao wamepitia shida ya vidonda kwa muda mrefu na ni muhimu kufanyiwa upasuaji.
Alisema wagonjwa pia walio na midomo iliyopinduka na ingetaka upasuaji wa dharura.
Alisema watazuru Meru kufanya upasuaji huo.
“Huu ni mpango wa kupongezwa pakubwa kwa sababu utaendeshwa na wataalam wenye ujuzi wa hali ya juu kuhusu upasuaji,” alisema Prof Waudo.
Alieleza kuwa mradi huo utaendeshwa katika kitengo cha masomo ya kiafya katika Kituo cha Sayansi za Afya ambacho kina vitengo vitan , chini ya uangalizi wa Dkt Joseph Njuguna ambaye ndiye msimamizi mkuu.
Vitengo hivyo ni Medical Pharmacy, Nursing, Public Health, Clinical Nursing, na Pharmacy.
Alisema lengo lao kuu pia litakuwa kufanya utafiti wa kina na kuhifadhi matokeo yake kwa njia ya kipekee ili kufanyiwa majaribio siku zijazo.