Michezo

Spurs, Palace ni kijasho ligi ya EPL

February 23rd, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KLABU za Tottenham, Bournemouth, Crystal Palace na Newcastle zinalenga kuimarisha rekodi zao nzuri dhidi ya Burnley, Wolves, Leicester na Huddersfield katika mechi za Ligi Kuu mtawalia hivi leo Jumamosi.

Tottenham ya kocha Mauricio Pochettino inazuru uwanjani Turf Moor ikitafuta kudumisha rekodi ya kutoshindwa na Burnley hadi mechi 10.

Vijana wa Pochettino walipepeta Burnley 3-0 kupitia mabao ya Harry Kane walipozuru Turf Moor msimu uliopita na pia kuwakung’uta 1-0 kupitia bao la dakika ya mwisho kutoka kwa Christian Eriksen walipokutana katika nusu ya kwanza msimu huu.

Spurs, ambayo inasakatiwa na Mkenya Victor Wanyama, inashikilia nafasi ya tatu. Ina fursa nzuri ya kukwamilia nafasi hiyo na kuweka hai matumaini ya kupigania taji ikichapa nambari 15 Burnley, ambayo inatarajiwa kujituma zaidi ili kujiondoa karibu na maeneo hatari ya kutemwa zinaposalia chini ya mechi 10 msimu 2018-2019 utamatike.

Burnley ya kocha Sean Dyche iko alama tatu nje ya mduara hatari. Mwingereza Kane amekuwa nje akiuguza jeraha, ingawa huenda akarejea katika mchuano huu ambao Spurs inatarajiwa kutegemea mchana-nyavu matata kutoka Korea Kusini Son Heung-min.

Burnley imekuwa ikipata magoli yake mengi kupitia Chris Wood, ambaye ameona lango mara tatu katika mechi tatu zilizopita. 
Nambari 11 Bournemouth ilichapa Wolves inayoshikilia nafasi ya saba mara tatu mfululizo 2-1 kabla ya kunyamazishwa 2-0 zilipokutana mara ya mwisho mwezi Desemba 2018.

Bournemouth inauguza vichapo dhidi ya Liverpool (3-0) na Cardiff (2-0). Wolves haijapoteza katika mechi saba zilizopita.
Nambari 13 Palace inafurahia kupepeta Leicester katika mechi tatu zilizopita.

Motisha

Itakuwa na motisha hata zaidi ya kufukuzia ushindi mwingine dhidi ya nambari 12 Leicester ambayo haijashinda katika mechi tano mfululizo ligini. 
Newcastle, ambayo inashikilia nafasi ya 16, ilibwaga wavuta-mkia Huddersfield 1-0 katika mechi mbili zilizopita. Huddersfield, ambayo ililemea Newcastle 1-0 Agosti 20 mwaka 2017, haina ushindi katika mechi 14 zilizopita.

Mechi kubwa wikendi hii itakuwa kati ya mahasimu wakubwa Manchester United na Liverpool hapo kesho Jumapili.