Michezo

NI KIVUMBI: Manchester United pembamba wakizuru PSG kwa marudiano ya UEFA

March 6th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

PARIS, UFARANSA

LICHA ya kichapo cha 2-0 ambacho Manchester United walipokea kutoka kwa PSG katika mkondo wa kwanza ugani Old Trafford, kocha Ole Gunnar Solskjaer anaamini vijana wake wana uwezo wa kubatilisha matokeo hayo leo Jumatano usiku.

Mshindi wa mikondo miwili atatinga robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Tutaingia uwanjani kushambulia kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, huku tukilenga ushindi wa kutuwezesha kusonga mbele,” alisema raia huyo wa Norway.

Hata hivyo, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itakuwa bila nyota wake tegemeo, Paul Pogba kutokana na marufuku ya kadi mbili za manjano.

Baadhi ya wachezaji wa Manchester United wafanya mazoezi Machi 5, 2019, katika uwanja wa The Parc des Princes jijini Paris, siku moja kabla ya mechi ya mkondo wa marudiano dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG). Picha/ AFP

Kadhalika, huenda Anthony Martial akakosa kuwa kikosini, pamoja na viungo Ander Herrera na Nemanja Matic wanaouguza majeraha.

Wengine wanaokabiliwa na majeraha ni Juan Mata na Antonio Valencia.

Mastaa kukosekana

Kutokana na kukosekana kwa mastaa kadhaa kikosini, mashabiki wengi wanaipatia Man-United nafasi finyu, ingawa Solskjaer aliyeiwafungia bao la ushindi na kuwasaidia kutwaa ubingwa wa 1999 dhidi ya Bayern Munich anaipigia debe timu yake.

“Hatuogopi chochote. Tumekuwa tukipata matokeo mema ugenini na hata nyumbani. Tutapigana vikali hadi dakika ya mwisho,” alisema Solskjaer kupitia kwa mtandao wa klabu yake.

“Tunaelewa si rahisi kuondoka na chochote ugani Parc des Princes baada ya wapinzani wetu kucheza vizuri katika mkondo wa kwanza kutuzidi, lakini kila mchezaji anaelewa umuhimu wa mechi hii,” aliongeza.

“Itakuwa bora zaidi iwapo tutalenga ushindi wa 4-2, badala ya ushindi wa 2-0. Tunafaa twende mapumzikoni tukiwa kifua mbele. Ikiwa tutabahatika kuongoza kwa 1-0 kufikia wakati wa mapumziko, chochote chaweza kutokea katika kipindi cha pili.”

“Katika mkondo wa kwanza, walitawala mechi ikielekea kumalizika, lakini leo, tutajitahidi tuwezavyo huku tukimtegemea Victor Lindelof baada ya kiwango chake kuimarika. Tunaweza kupata bao moja mapema, na tuzidishe mashambulizi na kupata mengine ya ushindi, dakika 15 au 20 za mwisho,” alisema.

“Kiwango cha Lindelof kimeimarika zaidi baada ya kurejea, wakati tukiwatarajia Phil Jones na Chris Smalling kutamba katika ngome ya ulinzi,” aliongeza.

Man United wameshinda mechi zao zote nane za ugenini katika mashindano yote tangu ujio wa Solkjaer ambaye amepewa mkataba wa muda mfupi baada ya Jose Mourinho kutimuliwa ugani Old Trafford.

“Nina imani na wachezaji wangu ambao wameamua kucheza kwa nguvu zote wakilenga kuibwaga PSG na kusonga mbele katika UEFA. Kila mtu amejiandaa vyema kwa mechi ya Jumatano,” alisema Solkjaer.

“Wachezaji wamekuwa wakicheza vizuri ugenini na huenda tukafaulu kutokana na hilo. Tutakuwa tukijiamini,” aliongeza.

Solskajaer amesema anavyoamini, vijana wake wanaweza kuzinduka katika michuano hii kutokana na ushindi walioupata dhidi ya Southampton katika pambano la EPL.

Katika mechi hiyo, mshambuliaji Romelu Lukaku alifunga mabao mawili, huku kiungo mahiri Andreas Pereira akipachika moja katika ushindi wao wa 3-2 ugani Old Trafford.

Hata hivyo, Manchester United hawatarajiwi kuvuma mbele ya masogora wa kocha Thomas Tuchel ambaye anatarajiwa kushusha kikosi imara kitakachowajumuisha Angel Di Maria, Verratti, Draxler na Mbappe.

Manchester wanahitaji kufanya kila jitihada watakaposhuka ugani Parc des Princes baada ya kocha wao kudai kwamba uhusiano miongoni mwa wachezaji wake umeimarika kwa kii kikubwa.

“Tunafahamu itakuwa ni mechi ngumu, lakini hakuna anayefahamu ugumu huo utakuwaje. Tumewahi kucheza mechi ngumu aina hii na kufaulu. Kumbuka klabu hii ina historia kubwa ya kubadili matokeo,” alisema.