Makala

Ujenzi wa makazi ya mbuzi, hasa wa maziwa mjini

March 13th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU       

MBUZI wanafugwa kwa madhumuni mbalimbali kama vile; nyama, maziwa na ngozi, na hata kuuzwa ili kujiinua kimaendeleo.

Idadi kubwa ya wafugaji wa wanayama hawa iko mashambani, kwa sababu ya kuwepo kwa mashamba makubwa. Hata hivyo, kuna baadhi ya waliofanikisha shughuli hii maeneo ya mijini licha ya upungufu wa ardhi.

Bw John Karira ni mmoja wao, ambapo anawafugia mjini Karatina, Nyeri.

Lengo lake hasa ni kupata maziwa, ikizingatiwa kuwa maziwa ya mbuzi nchini ni adimu, lakini adhimu.

Yana ukwasi wa madini ya Potassium, Calcium na Protini.

Kadhalika, kiwango chake cha mafuta ni cha chini mno.

Mfugaji huyu anasema mbuzi ni mifugo rahisi kutunza, ukilinganishwa na wengine.

Mbuzi wawili. Picha/ Sammy Waweru

Anatia moyo wenye ari ya kuwaweka mjini, akieleza kwamba hawahitaji nafasi kubwa ya ardhi.

“Gharama ya kuwafuga, kuanzia makazi, lishe na matunzo ni ya chini mno. Wanahitaji muda mfupi kuwahudumia,” anadokeza Bw Karira ambaye kando na kufanya kilimo cha mbuzi ni afisa wa polisi, kitengo cha askari tawala (AP).

Ujenzi wa makazi

Anatoa mfano, ploti yenye ukubwa wa robo ekari mbali na kujengwa nyumba, egesho na bustani ndogo, ina uwezo wa kuundwa makazi ya mbuzi yenye urefu wa futi 30, 8 upana na 13.7 kuenda juu, kwa kutumia mbao.

Aidha, makazi yenye vipimo hivi yanasitiri karibu mbuzi 20.

Unashauriwa kuyaunda kuanzia futi tatu kutoka ardhini ili kuzuia viroboto kushambulia mbuzi.

Viroboto hutatiza mifugo. Kwenye kipimo cha futi 13.7 kuenda juu, ondoa futi 3 kutoka ardhini. Pima futi 6.7 na hii inatosha kusitiri mbuzi.

Futi nne zilizosalia kuenda juu, ni za kuhifadhi lishe kisha yaezekwe kwa mabati.

Sehemu ya kuwatilia mlo isiwe hoja, kwani katika urefu wa futi 30, unapendekezwa kuondoa futi mbili kwa madhumuni yake.

“Sakafuni, mbao zisishikanishwe ili kuruhusu kinyesi na mkojo kutoka hususan wakati wa usafi,” ashauri Karira.

Mfugaji pia anahimizwa kujengea vibuli, vikembe wa mbuzi, makazi yao maalumu pamoja na eneo la kupumzika, kulishwa na kunyweshwa au kutiliwa maji.

Kauli ya mfugaji huyu inawiana na ya Joseph Mathenge, anayefuga mbuzi wa maziwa Kiambu.

“Nilichagua ufugaji wa mbuzi kwa kuwa ni rahisi mno. Gharama yake ni ya chini, lishe huwatilia asubuhi na jioni,” aeleza Bw Mathenge.

Usafi na lishe

Usafi wa makazi na mazingira ndio kiini cha ufanisi katika ufugaji wowote ule.

“Sawa na kuku, mbuzi, kondoo na ng’ombe, usafi wa makazi yao uwe wa hadhi ya juu ili kudhibiti vimelea na magonjwa,” anasema Simon Mwara, mfugaji wa mbuzi na kuku Kiambu. Mbali na mazingira, usafi wa chakula, maji na wanamotiliwa uwe wa daraja la juu.

Mbuzi hula nyasi aina ya Hay, chakula maalumu cha mifugo, Lucerne na Boma Rhodes.

“Mifugo wanapaswa kulishwa nyasi zilizokauka ili kuwaepushia athari za wadudu na maambukizi ya magonjwa yanayosababishwa na nyasi za kijani,” asisitiza Bw Andrew Ondijo, mtaalamu wa mifugo.

Nyasi zilizokauka pia huwawezesha kunywa maji kwa wingi, kiungo hiki kikiwa muhimu katika uundaji wa maziwa.

Faida

Mbuzi hasa aina ya Alphine, waliotunzwa kitaalamu huzalisha kati ya lita tatu hadi nne kwa siku.

Maeneo ya mijini kama vile Nairobi, Nyeri na Kiambu, lita moja ya maziwa haya inagharimu Sh200.

Hii ina maana kuwa mfugaji akiweka zingatio kwa wale wa maziwa, mmoja atamtuza Sh800 kila siku.

Akiwa na watano wa kukama, atatia mfukoni Sh4,000 na kwa kukokotoa kitita cha Sh120,000 kwa mwezi.

Wafugaji hawa na ambao wamefanikisha ufugaji wa mbuzi mjini, kwa kauli moja wanakubaliana kwamba ni rahisi kufugia wanyama hawa katika kipande kidogo cha ardhi.

“Hoja isiwe nafasi ya kuwaweka, ila kupata soko la mazao. Soko la mazao yake hasa maziwa ni mithili ya mahamri moto,” wanasisitiza.