Habari Mseto

200 watapeliwa maelfu kupitia jina la Naibu Rais

January 1st, 2020 2 min read

Na WAWERU WAIRIMU

WAKAZI zaidi ya 200 kutoka Isiolo wanakadiria hasara baada ya kutapeliwa na mwanamme aliyewaahidi kuwasaidia kukutana na Naibu Rais William Ruto jijini Nairobi ili kujadili utekelezaji wa ripoti ya Building Bridges Initiative (BBI).

Wakazi hao waliojawa na ghadhabu walieleza wanahabari kwamba, walikuwa wamelipa kiasi cha Sh2,300 kila mmoja wao ili kugharamia usafirishaji na utengenezaji wa T-Shirt mnamo Jumapili jioni kabla ya safari iliyopangiwa kufanyika Jumatatu asubuhi.

Hata hivyo, waligundua kwamba walikuwa wamenaswa kwenye mtego wa mlaghai huyo aliyetambulishwa kama Bw Peter Mwangi baada ya kusubiri kwa saa sita bila kupokea T-shirt wala basi zilizopaswa kuwasafirisha kuwasili ili kuwachukua.

Wakazi hao walisema Bw Mwangi alikuwa amewaeleza kwamba, mkutano huo ulikuwa wa kujadili ripoti ya BBI iliyozinduliwa majuzi huku wakipanga mikakati ya jinsi ya kuwa sehemu ya kundi la kumfanyia kampeni Dkt Ruto katika azma yake ya urais 2022.

Bw David Muthamia, mmoja wa wahasiriwa hao, alisema Bw Mwangi vilevile aliwaahidi kwamba wangepata marupurupu ya Sh10,000 kila mmoja baada ya mkutano huo.

“Ulikuwa mpango wa kuvutia mno na hatungefikiri kamwe ungegeuka ulaghai. Tulikuwa tujadili jinsi ya kumuunga mkono Naibu Rais katika kampeni za 2022 kulingana na Mwangi.”

“Mwanamme huyo alitujia na akatueleza kuwa kukutana na Naibu Rais kungebadilisha maisha yetu,” alisema Bw Muthamia.

Bi Joyce Mwari aliyekuwa amekopa hela kutoka kwa rafiki alisema walikutana na mwanamme huyo Jumapili jioni na wakaahidiwa kuwa T-shirt hizo zilizowekwa nembo ya Dkt Ruto zingewasilishwa Jumatatu asubuhi kabla ya kuanza safari ya kuelekea Nairobi.

Hasira

Alisema walipangiwa kuondoka saa kumi alfajiri na walipoulizia, Mwangi alisisitiza kila mara kuwa basi hizo nne za shule zilizokuwa zimekodishwa zilikuwa zikiwekwa mafuta katika mji jirani wa Isiolo.

“Tumekuwa tukisubiri hapa kwa zaidi ya saa tano tukitumai kwamba mwanamume huyo atajitokeza lakini yaonekana tumehadaiwa,” alisema mfanyabiashara huyo akiwa amejawa na hasira.

Kundi hilo baadaye liliripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Isiolo na kuwasihi polisi kumsaka mshukiwa na kusaidia kupata hela hizo zilizoibiwa za kiasi cha Sh483,000.

“Tunatoa wito kwa polisi kumsaka mshukiwa kwa kututapeli na kumchafulia jina Naibu Rais,” alisema Bi Esther Makena.

Idadi kubwa ya wahasiriwa waliepuka kuzungumza na wanahabari kutokana na hali ya kutoamini kwamba kwa kweli walikuwa wamelaghaiwa.

Tulipowasiliana naye, Bw Mwangi alidai kwamba alikuwa amepatiwa kandarasi na kundi la kutoa ufadhili kwa wanajamii linaloitwa “Power” kukusanya wakazi kutoka kaunti hiyo, ili wakutane na Dkt Ruto, lakini mwenyekiti wa kitaifa aliyestahili kuchukua barua rasmi alitoweka baada ya kupokea maelfu kutoka kaunti zote 47.