Makala

2018: Mataifa yalihalalisha bangi huku Kenya ikiilaani

December 24th, 2018 3 min read

 CECIL ODONGO na CHARLES WASONGA

HUKU Kenya na mataifa mengine yakiendelea kuichukua bangi kama dawa ya kulevya ambayo ni marufuku kupanda mmea wake ama kuvuta, mataifa makubwa makubwa duniani hadi kufikia mwisho wa mwaka huu yalihalalisha matumizi ya bangi nchini mwao.

Raia wa mataifa hayo sasa hawatakuwa na kizuizi chochochote wanapofaidi uhondo, raha na msisimko unaoandamana na ‘kupiga puff’ dawa hiyo ya kulevya ambayo ukipatikana nayo hapa Kenya basi utakabiliwa na adhabu kali za kisheria mahakamani itakayokukutia majuto makubwa sana.

Hapa nchini kumekuwa na pendekezo la kuhalilishwa bangi lililoasisiwa na Mbunge wa Kibera Ken Okoth, mwanauchumi David Ndii na mwanawe wa kiume wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga, Raila Odinga Junior. Hata hivyo pendekezo hilo limepokelewa kwa hisia mseto miongoni mwa raia na madaktari, wawili hao wakiunga pendekezo lao kwa kusema kwamba bangi ina manufaa ya kiafya kwa mtumiaji wake ama ni tiba kwa baadhi ya maradhi sumbufu yanayoathiri akili ya binadamu.

Bw Okoth vilevile amepanga kuwasilisha mswada bungeni wa kuidhinisha utumiaji wa bangi japo watoto hawataruhusiwa kuitumia jinsi ilivyo kwa vileo/pombe na sigara zinazouzwa tu kwa waliofikisha umri wa miaka 18 na zaidi.

Tukirejea mada hii, Taifa la hivi punde kuchukua mkondo huo ni Mexico ambayo mnamo Jumatano 19 Disemba mwaka huu ilikumbatia uhalalishaji wa dawa hiyo ya kulevya.

Hii ni kufuatia hatua ya mahakama ya upeo wa juu ya taifa hilo kutoa uamuzi unoridhia upandaji, umiliki na uvutaji wa bangi kama njia ya kujiburudisha chini ya haki ya uhuru wa kila raia iliyonakiliwa kwenye katiba ya nchi hiyo. Uamuzi huo wa kihistoria ulipigiwa kura 4-1 na benchi ya majaji watano wa mahakama hiyo yenye mamlaka makubwa zaidi nchini Mexico.

Majaji hao walisema kwamba kuvuta bangi imeamrishwa chini ya haki ya ‘Uhuru wa maendeleo ya mtu binafsi ‘ katika katiba ya Mexico wala uvutaji huo haufai kuchukuliwa kama kosa la uhalifu.

Hapa Barani Afrika, Afrika Kusini mwezi Septemba ilihalalisha matumizi ya bangi. Mahakama ya kikatiba nchini humo kupitia uamuzi wa majaji uliamrisha bunge la taifa hilo kutunga sheria zitakazoongoza na kuruhusu matumizi ya kibinafsi ya bangi kwa muda wa miezi 24 ijayo.

Ingawa hivyo, imebainika kwamba nchi nyingi zimeanza polepole kujiondoa katika tabia ya zamani ya kuwakabili vikali watu wanaotumia dawa hiyo ya kulevya. Adhabu ya vifungo vya miaka mingi au maisha vimetelekezwa kinyume na miaka ya nyuma ambapo kupatikana na mihadarati ilikuwa kama kujichimbia kaburi.

Canada pia mwaka huu ilijunga na ‘wanabangi’ na ikawa ya kwanza kati ya mataifa yanayounda muungano wa G7 kuruhusu uvutaji wa bangi kujiburudisha. Hata hivyo, sheria hiyo iliandamana na masharti makali ya kila nyumba kutokubaliwa kumiliki bangi zaidi ya kilo 30 huku ikiruhusiwa kupanda mimea minne tu ya ‘cannabis Sativa’ (jina la kibayolojia ya bangi).

Uruguay ndiyo ilikuwa taifa la kwanza duniani kuidhinisha upanzi wa bangi, usambazaji na matumizi yake.

Kulingana na sheria ya nchi hiyo, wananchi na wenyeji wanaruhusiwa kununua gramu 40 ya bangi pekee kwa mwezi kutoka kwa maduka ya dawa/famasia, au waikuze nyumbani mwao au kuungana katika makundi ili kushiriki upanzi wake.

Serikali ya Uruguay vilevile imezipa kampuni mbili leseni za kushiriki upanzi wa bangi na kuzisambaza nchini humo.

Nchi hizo ni Chile iliyohalilisha bangi mwaka wa 2015, Colombia ikafuata mwaka wa 2016 kisha Argentina na Peru mwaka jana.

Barani Uropa Austria, Croatia, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ugiriki , Italia, Macedonia, Poland, Romania na Slovenia zimeidhinisha matumizi ya bangi ila katika sababu zilizo na mashiko na zenye ulazima za kimatibabu.

Nchi ya Korea Kaskazini nayo haijali au kuhusika kivyovyote iwapo raia wake amepanda wala kutumia bangi. Katika taifa hilo la kikomunisti kila raia yu huru huria kupanda bangi kiwango anachotaka.

Jamaica na Uswisi nayo yanasheria legevu kuhusu umiliki wa bangi ila hazijali wala kuadhibu raia wanaotumia au kupanda kiasi cha ‘wastani’ cha bangi.

Iwapo Kenya na mataifa mengine barani yatakumbutia uhalalishaji wa bangi ni muda tu utakaosema japo kwa sasa patikana na bangi uone!