Makala

2018: Mgomo wa siku 76 ulisambaratisha masomo ya wanafunzi 600,000

December 28th, 2018 2 min read

Na WANDERI KAMAU

MWAKA huu utakuwa kama kumbukumbu kuu katika vyuo vikuu nchini, baada ya wahadhiri kushiriki katika mgomo uliodumu kwa siku 76.

Mgomo huo ulihusu utata wa kuongezwa mishahara kwa wahadhiri kwenye Mwafaka wa Malipo wa 2017-2021.

Muungano wa Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (UASU) uliamua kumaliza mgomo huo mnamo Machi 17 baada ya mazungumzo yaliyojiri kwa muda mrefu na Wizara ya Leba katika makao yake makuu. Mazungumzo hayo yaliongozwa na Bi Hellen Apiyo, aliyeteuliwa kuwa mpatanishi wa pande hizo mbili.

Wahadhiri walianza mgomo huo mnamo Desemba 2017 kwa kukataa Sh3.6 bilioni zilizotolewa na serikali kama sehemu ya Sh10 bilioni, walizotaka kuongeza mishahara yao. Wahadhiri walikuwa wakishinikiza nyongeza ya mishahara yao hadi asilimia 60. Hilo lilimaanisha kwamba mhadhiri angepata mshahara wa hadi Sh800,000 huku wa kiwango cha chini zaidi akipata Sh263,000.

Mgomo huo uliwaathiri zaidi ya wanafunzi 600,000 ambao wamo katika vyuo vikuu 31 vya umma.

Katibu Mkuu wa UASU Constantine Wasonga alisema kwamba walimaliza mgomo huo ili kutoa muda zaidi kwa mazungumzo.

Vile vile, waliamua hilo kwa kujali maslahi ya maelfu ya wanafunzi ambao walikuwa wakiendelea kuteseka kwa kutohudhuria masomo.

Licha ya kumaliza mgomo huo kighafla, iliibuka baadaye kwamba wahadhiri waliamua kurejea kazini baada ya serikali kutishia kuwafuta kazi.

Serikali pia iliamua kutekeleza nyongeza hiyo, ingawa kwa muda wa miaka minne, ambapo wahadhiri watatengewa jumla ya Sh38 bilioni.

Wahadhiri waliozungumza bila kutaka kutajwa walisema kwamba walishajiishwa kurejea kazini na wakuu wa vyuo kwa kutia saini barua maalum inayoonyesha kwamba hawatafanya hivyo bila kutoa masharti yoyote.

Wale waliokataa agizo hilo walitishiwa kufutwa kazi. Ripoti ziliibuka kwamba wahadhiri 35 katika Chuo Kikuu cha Nairobi ambao waliasi maagizo hayo walipewa likizo ya lazima, huku wengine zaidi ya 1,200 wakikosa kulipwa mishahara yao ya mwezi Machi.

Iliibuka pia kwamba vyuo vikuu viliwaagiza viongozi wa wanafunzi kuandaa vikao ili kuwashinikiza wahadhiri kurudi kazini. Baada ya shinikizo kuongezeka, vyuo vikuu vya umma kama Kenyatta, Moi, JKUAT kati ya vingine vililazimika kuwaagiza wahadhiri na wafanyakazi wa idara zingine kurejea kazini.

Licha ya kumaliza mgomo huo, sharti jingine kwa wahadhiri lilikuwa kuondoa kesi ambayo walikuwa wamewasilisha katika Mahakama Kuu kupinga utathmini wa mishahara na Tume ya Kutathmini Mishahara (SRC).