Habari MsetoSiasa

2019: Jinsi kitumbua cha Gavana Sonko kiliingia mchanga

December 24th, 2019 2 min read

Na COLLINS OMULO

VITUKO vya kila aina kama vile kupiga ngumi ukuta, kumpigia simu Rais Uhuru Kenyatta huku akiwa ameweka sauti ya juu na kuonekana kuwa mtetezi wa watu alipokuwa seneta, vilimfanya Gavana Mike Sonko kuwa kipenzi cha wakazi wa Nairobi.

Bw Sonko alipata kura nyingi jijini Nairobi kuliko Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi mkuu wa 2017 ambapo alichaguliwa kuwa gavana wa pili wa Nairobi.

Miaka miwili baada ya kushika hatamu za uongozi wa jiji, masaibu tele yameanza kumwandama.

Hata baada ya kushinda tuzo nne katika kipindi cha mwaka mmoja kwa kuonyesha ‘uongozi bora’, maafisa wa uchunguzi kutoka Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) hawakumsaza.

Kiongozi huyu wa Kaunti ya Nairobi sasa anakabiliwa na kesi inayomhusisha na wizi wa mamilioni ya fedha za umma.

Mahakama imezuia Gavana Sonko kurejea ofisini hadi pale kesi inayomkabili itakaposikilizwa na kuamliwa.

Baadhi ya madiwani wa Kaunti ya Nairobi wameanzisha harakati za kutaka kumtimua Gavana Sonko.

Gavana aliyejivunia kuwa mwandani wa karibu wa Rais Kenyatta na Naibu wa Rais William Ruto, sasa anaonekana kutolewa pumzi na ushawishi wake kufifia.

Hakuwepo uwanjani Nyayo, Nairobi wakati wa maadhimisho ya sherehe za Jamhuri.

Miezi michache kabla ya kunaswa, Bw Sonko alikuwa akiponda raha kutoka nchi moja hadi nyingine huku akirekodi video akisakata densi katika maeneo ya burudani.

Sasa jiji la Nairobi linaonekana mahame huku likizongwa na marundo ya takataka, msongamano wa magari, wachuuzi wametapakaa kote, uhaba wa maji upo, miradi imekwama na sasa sakata ya wizi wa mamilioni ya fedha.

Kaunti ya Nairobi haijakuwa na naibu gavana kwa miaka miwili sasa na hakuna katibu wa kaunti.

Gavana Sonko amekuwa akihamisha mawwaziri mara kwa mara; Waziri wa Fedha alitimuliwa na waziri wa Afya alisimamishwa kazi. Wizara ya Mpangilio wa Jiji imelemazwa baada ya Bw Sonko kusimamisha kazi maafisa 14 mnamo Septemba.

Mnamo Novemba, Bw Sonko alishinda Tuzo ya Gavana Bora wa mwaka wa 2019. Mnamo Agosti alituzwa digrii ya heshima na Chuo Kikuu cha European Digital katika Chuo Kikuu cha Dubai kwa mchango wake katika kuleta mabadiliko katika jamii.

Mnamo Februari aliteuliwa kuwa balozi wa Matendo Mema na shirika la Good Deeds Global la nchini Israeli kutokana na ukarimu wake kwa watu wenye mahitaji.

Mnamo Oktoba, Nairobi ilibwaga majiji mengine 105 na kutawazwa mshindi wa tuzo ya Usawa wa Kiuchumi na Kijamii katika hafla ya Milan Pact Awards 2019.

Hata hivyo, Bw Sonko amekuwa akisisitiza kuwa hatua yake ya kuwasimamisha kazi kiholela maafisa wa serikali yake haiwezi kuathiri utoaji wa huduma jijini.

Masaibu ya Sonko yalianza wakati ambapo aliyekuwa waziri wa Elimu wa Kaunti ya Nairobi Janet Ouko alipojiuzulu ghafla mnamo Januari mwaka huu.

Mvutano baina ya Bw Sonko na Bi Ouko ulifichua uozo katika serikali ya kaunti na kuwafanya maafisa wa uchunguzi kuanza kunyemelea uongozi wa jiji la Nairobi.

Gavana Sonko aliandikia barua Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) na EACC akielezea jinsi wizi umekolea katika hazina ya utoaji ufadhili wa masomo.

Maafisa wa EACC mnamo Mei walimnasa Kaimu Katibu wa Kaunti Bi Pauline Kahiga kwa madai ya kuficha stakabadhi muhimu zinazohusiana na uchunguzi uliokuwa ukiendelea.

Mnamo Septemba Gavana Sonko alialikwa kufika katika Makao Makuu ya EACC kuhusiana na tenda ya ukusanyaji wa takataka na hapo ndipo kitumbua kiliingia mchanga.