HabariSiasa

2020: Demokrasia ilivyodorora Afrika kupitia chaguzi mbalimbali

December 23rd, 2020 4 min read

Na LEONARD ONYANGO

MATAIFA tisa yalifanya uchaguzi wa urais mwaka huu barani Afrika licha ya kuwepo kwa janga la virusi vya corona ambalo limetikisa ulimwengu.

Lakini baadhi ya chaguzi ziligubikwa na madai ya kuwepo kwa udanganyifu, vitisho kwa viongozi wa upinzani na vurugu hivyo kutia doa demokrasia barani Afrika.

Mataifa yaliyoandaa uchaguzi wa urais mwaka huu ni Malawi, Togo, Tanzania, Seychelles, Guinea, Ghana, Cote d’Ivoire, Burundi na Burkina Faso.Nchi nyingine kama vile Benin, Cameroon, Misri, Mali, Namibia na Niger zilifanya uchaguzi wa maseneta, wabunge au serikali za miji.

Tanzania

Rais John Pombe Magufuli aliapishwa kuongoza Tanzania kwa muhula wa pili mnamo Novemba 5, mwaka huu. Rais Magufuli aliapishwa licha ya kuwepo kwa lalama kutoka kwa vyama vya upinzani kuhusu kuwepo kwa visa vya udanganyifu katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28.

Rais Magufuli aliibuka mshindi baada ya kupata asilimia 84 ya kura zilizopigwa huku mshindani wake mkuu Tundu Lissu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema) akipata asilimia 13.

Chama cha Mapinduzi (CCM) chake Rais Magufuli kilishinda viti vya ubunge katika maeneobunge 256. Chama cha ACT- Wazalendo kilifuatia kwa wabunge wanne, Civic United Front (CUF) kilifuatia wabunge watatu na Chadema kilipata mmoja.Katika uchaguzi wa 2015, CCM ilishinda ubunge katika maeneobunge 206, CUF ilipata viti 29, Chadema ilikuwa ya tatu kwa viti 26 huku ACT-Wazalendo na NCCR- Mageuzi vikipata kiti kimoja kimoja.

Upinzani ulidai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na visa vya wizi wa kura – madai ambayo yaliungwa mkono na mataifa mbalimbali, ikiwemo Amerika.

Kabla ya uchaguzi kulikuwa na madai ya kugandamiza vyombo vya habari na kusitisha huduma za mtandao.Viongozi wa upinzani, wakiwemo Lissu na Zitto Kabwe wa chama cha ACT- Wazalendo walikamatwa na kisha kuachiliwa. Mara baada ya uchaguzi, Lissu alipewa hifadhi katika ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania.

Baadaye, Lissu alienda kuishi uhamishoni Ubelgiji.Aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema alikimbilia mafichoni nchini Kenya na kisha kwenda kuishi uhamishoni Canada kwa kuhofia maisha yake na familia.Mwezi uliopita, mataifa mbalimbali, ikiwemo Uingereza yalitaka kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusiana na uchaguzi wa Oktoba 28.

Waziri wa masuala ya Afrika James Duddridge alisema kwamba Uingereza ilishangazwa na ripoti za ghasia na kiwango cha juu cha maafisa wa polisi katika vituo vya kupigia kura ikiwemo suala zima la kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani, kujazwa kwa kura katika masanduku ya kura na kuzuiliwa kwa mawakala wa vyama vya upinzani kuingia katika vituo vya kura.

Cote d’Ivoire

Rais Alassane Ouattara alivunja rekodi mwaka huu kwa kuchaguliwa na asilimia 94 ya wapigakura katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 31.Uchaguzi huo ulifanyika hata baada ya maelfu ya raia wa nchi hiyo kuandamana kupinga Ouattara kuwania kwa muhula wa tatu.

Wawaniaji wa vyama vya upinzani; Henri Konan Bedie na Pascal Affi N’Guessan walisusia uchaguzi huo huku wakidai kuwa Ouattara alikiuka katiba kwa kuwania urais kwa muhula wa tatu baada ya kukamilisha mihula yake miwili.Baada ya kupigwa kwa kura, polisi walivamia nyumbani kwa Bedie na kufyatua risasi hewani.

Polisi pia walikamata maafisa wa chama cha Bedie kwa kushinikiza serikali kuandaa uchaguzi upya na kutishia kuunda serikali yao.Uhasama baina ya Rais Ouattara na Bedie ulianza miaka 30 iliyopita ambapo walishindana katika juhudi za kutaka kumrithi rais wa kwanza wa nchi hiyo Felix Houphouet-Boigny.

Mwezi uliopita, shirika la kutetea haki za kibinadamu, Amnesty International, lilisema kuwa serikali iliruhusu genge la watu waliokuwa na mapanga, marungu na silaha butu kushambulia waandamanaji waliokuwa wakipinga ushindi wa Rais Ouattara jijini Abidjan.

Togo

Naye, naye Rais wa Togo Faure Gnassingbe alitangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Februari 22 baada ya kupata asilimia 72 ya kura zilizopigwa.

Gnassingbe ambaye amekuwa mamlakani tangu 2005, alitangazwa mshindi ndani ya saa 24 baada ya shughuli ya kupiga kura kumalizika huku upinzani ukidai kuwa uchaguzi ulikumbwa na visa vya udanganyifu.

Kulingana na matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi, aliyekuwa waziri mkuu Agbeyome Kodjo alipata asilimia 18 ya kura huku mwaniaji wa chama cha National Alliance for Change (ANC) Jean-Pierre Fabre, aliibuka katika nafasi ya tatu kwa asilimia tano ya kura.

Mashirika ya kijamii yalidai kwamba kulikuwa na visa vya wizi wa kura. Wawaniaji wa vyama vya upinzani walipuuzilia mbali matokeo hayo huku Kodjo akijitangaza mshindi.

Gnassingbe alitwaa uongozi wa Togo baada ya baba yake Gnassingbe Eyadema aliyeongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 38 kufariki dunia 2005.

Malawi ndiyo nchi ambayo ilionekana kuiondolea Afrika aibu ya kugandamiza demokrasia baada ya mahakama ya katiba kubatilisha matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Mei mwaka jana, ulikumbwa na visa vya wizi.Mahakama ilibaini kuwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Peter Mutharika aliiba kura na kuagiza kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Majaji wa mahakama ya katiba walikuwa wakisafirishwa kwa kutumia magari ya jeshi ili kulinda maisha yao.Uchaguzi huo ulirudiwa Juni, mwaka huu na mwaniaji wa chama cha upinzani Lazarus Chakwera akaibuka mshindi kwa asilimia 58 ya kura zilizopigwa.

Gazeti la Economist lililo na ushawishi zaidi nchini Uingereza lilitaja Malawi kuwa nchi nambari moja iliyotetea misingi ya demokrasia duniani.

Ghana?Mwaniaji wa upinzani John Mahama, 62, amepinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 7 huku akidai kuwa kura zake ziliibiwa.

Tume ya uchaguzi ilitangaza Rais Nana Akufo-Addo wa chama cha New Patriotic Party (NPP) kuwa mshindi baada ya kupata asilimia 51.6 ya kura huku Mahama wa chama cha National Democratic Congress (NDC) akifuatia kwa asilimia 47.4. Vurugu zilishuhudiwa katika eneobunge la Techiman Kusini.

Chama cha NDC kilitaka uchaguzi urudiwe kikidai kuwa matokeo waliyo nayo yalionyesha kuwa hakuna mwaniaji aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zinazohitajika ili mwaniaji kuidhinishwa kuwa mshindi.

Mali

Mapinduzi ya serikali ya Ibrahim Boubacar Keita nchini Mali yalitia doa zaidi demokrasia barani Afrika.Keita alilazimishwa kujiuzulu baada ya kukamatwa na wanajeshi mnamo Agosti.

Akiwa amevalia barakoa, Keita ambaye aliongoza Mali kwa miaka saba, alitangaza kupitia vyombo vya habari kuwa aliamua kujiuzulu ili kuepusha umwakigaji wa damu.

Burkina Faso

Mnamo Novemba 26, Rais Roch Kabore alitangazwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika Novemba 22 hivyo kupata fursa ya kuongoza taifa hilo kwa muhula wa pili.

Waangalizi wa uchaguzi walisema kuwa uchaguzi huo wa Burkina Faso ulikuwa huru na wa haki japo baadhi ya wapigakura hawakujitokeza kutokana na hofu ya mashambulio ambayo yamekuwa yakitekelezwa na makundu ya magaidi wa mtandao wa Al-Qaida..