2020: Wizi serikalini, migomo na ukosefu wa ajira corona ikitafuna Kenya

2020: Wizi serikalini, migomo na ukosefu wa ajira corona ikitafuna Kenya

Na SAMMY WAWERU

Mshale wa kronomita ulipoashiria saa sita kamili za usiku Januari 1, Kenya iliungana na ulimwengu kuukaribisha mwaka wa 2020, shangwe, vifijo na nderemo zilizoandamana na fataki zikahinikiza anga mijini na vijijini.

Mamilioni ya Wakenya waliokuwa kwenye maeneo ya kuabudu, wengine ya burudani, vilabu na nyumbani, walikuwa na kila sababu ya kutabasamu kuuona mwaka mpya.

Ni mbwembwe zinazoshuhudiwa kila mwaka unapoanza, na 2020 hakuna binadamu angetabiri au kujua yale ambayo yangejiri ila Mwenyezi Mungu pekee.

Novemba 2019, tulikuwa tukisoma kwenye magazeti, kutazama runinga na kuskia redioni kuhusu ugonjwa wa Covid-19 uliochipuka mjini Wuhan, China.

Madaktari, Wanasayansi na wataalamu wa masuala ya afya waliutaja kama ugonjwa hatari, unaosababishwa na virusi vya corona, na unoua chini ya siku chache.

COVID-19: Ugonjwa unaosababishwa na virusi chipuka vya corona, CO ikiwa na maana ya corona, VI virusi na D tafsiri ya jina ugonjwa kwa Kiingereza, 19 mwaka ulipoibuka kwa mara ya kwanza.

Virusi vya corona vilianza kusambaa mataifa mengine ya ulimwengu kama moto wa nyika, maambukizi yakawa mamia, mamia ya maelfu na sasa ni mamilioni.

Maafa yalishuhudiwa na yanaendelea kushuhudiwa, afueni ya tiba ikibisha hodi baada ya chanjo kuzuia maambukizi zaidi kudaiwa kupatikana Uingereza.

Wakati tukiskia kuhusu virusi vya corona China, Waziri wa sasa wa Maji, Sicily Kariuki ndiye alikuwa Waziri wa Afya.

Mwanzoni mwa 2020, Rais Uhuru Kenyatta akamteua aliyewahi kuhudumu kama mbunge wa Mukurweini, Mutahi Kagwe kati ya 2002-2007, na seneta wa Nyeri 2013-2017, kumrithi Sicily Kariuki katika Wizara ya Afya.

Baada ya kupigwa msasa na bunge la kitaifa na uteuzi wake kuidhinishwa, Kagwe akala kiapo kuwa waziri mnamo Februari 28, 2020, siku chache kabla Kenya kuthibitisha mwenyeji wa Covid-19.

Machi 13, 2020, Waziri Kagwe alitangaza kisa cha kwanza nchini cha virusi vya corona. “Kisa cha kwanza ni Mkenya mwenye umri wa miaka 27…” akatangaza, taarifa iliyoshtua kila mwananchi kutokana na tuliyoskia kwenye vyombo vya habari.

Taifa kama Amerika lilionekana kulemewa na makali ya janga la corona, hivyo basi kila aliyeskia virusi hivi vikitajwa alijawa na kiwewe.

Machi 13, hata hivyo haikuwa siri tena, kwani Kenya ilithibitisha kuwa mwenyeji wa ugonjwa huu hatari.

Kilichofuata kikawa Waziri Kagwe na mawaziri wasaidizi wake kuandaa vikao vya kila siku na wanahabari Afya House, Nairobi, vikao vingine vikiandaliwa kaunti mbalimbali nchini.

Visa vya maambukizi na maafa vikaendelea kuongezeka, na kufikia sasa Kenya imeandikisha zaidi ya visa 96, 000 na maafa 1,665.

Wagonjwa waliothibitishwa kupona Covid-19 kufikia sasa ni 77,659, kwa mujibu wa takwimu za hivi punde za Wizara ya Afya.

Mwishoni mwa mwezi Machi, mambo yalipoonekana kuzidi unga, serikali iliamuru kufungwa kwa shule zote nchini na taasisi za elimu ya juu.

Zinatarajiwa kufunguliwa tena Januari 4, 2020, kwa mujibu wa amri ya Rais Uhuru Kenyatta, huku akisisitiza “lazima kila mwanafunzi arejee shuleni”.

Sheria na mikakati kusaidia kuzuia maenezi ya virusi vya corona zilizinduliwa, zikiwemo kuvalia maski maeneo ya umma, kutakasa mikono, mikusanyiko ya umma kupigwa marufuku, kafyu ya kitaifa, zile cha usafiri na uchukuzi, kati ya nyinginezo.

Ni athari za virusi vya corona zilizoonyesha makali yake katika sekta ya elimu, bila kusahau sekta ya biashara, utalii na uchukuzi, ambazo nusra ziyumbishwe.

Sekta ya afya nayo ndiyo imeonekana kulemewa kwa kiasi kikuu, ikiwa nguzo kuu kupambana na janga la corona nchini, wadau hasa wa miungano inayotetea wahudumu wa afya wakilaumu serikali kwa kuipuuza.

Ni hivi majuzi tu madaktari walishiriki mgomo wa kitaifa wakidai haki yao, na la mno kutaka kufadhiliwa vifaa (PPEs zikiwemo) kujikinga dhidi ya kuambukizwa Covid-19.

Hata hivyo, waliufutilia mbali baada ya mazungumzo na serikali na makubaliano kuafikiwa. Wauguzi nao wameapa kutositisha mgomo wao kote nchini hadi pale matakwa yao yatatekelezwa.

Virusi vya corona vimeua madaktari, wauguzi na wahudumu wengine wa afya walio katika mstari wa mbele kupambana na janga hili nchini.

Licha ya mahangaiko hayo, kilichoshtua taifa zaidi ni sakata ya ufisadi na ulafi katika idara ya afya wakati Covid-19 ikitesa.

Hii ni kutokana na uozo uliofichuliwa na mwanahabari mpekuzi wa NTV, Dennis Okari, kupitia makala ya Covid-19 Millionaires, yaliyoelezea fedha za kupambana na virusi vya corona pamoja na misaada, zilivyopunjwa na viongozi wahuni na wenye tamaa ya ubinafsi.

Msaada wa vifaa vya kupambana na Covid-19 vilivyopewa Kenya na wakfu wa Jack Maa, mfanyabiashara tajika China, pia vilichezwa shere.

Hayo yote yalitekelezwa wakati virusi vya corona vinaendelea kunoa makali, maelfu ya Wakenya wakipoteza ajira.

Huku ikiripotiwa kuna shehena ya chanjo ya Covid-19 inayotarajiwa kuingia nchini, matumaini ya raia 2021 ni uwe mwaka wa afueni kutokana na magumu na wazito waliyopitia.

You can share this post!

Unyama magaidi wakilipua ambulensi ya mjamzito

EACC yawazima Sonko na Baba Yao