Habari Mseto

Wafuatiliaji habari mitandaoni nusura wamle Miguna mzimamzima

March 16th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAKILI asiyeisha vituko Miguna Miguna alishambuliwa Ijumaa katika mitandao ya kijamii kwa kumdhalilisha Gavana wa Mombasa Hassan Joho.

Mwanasiasa huyu aliyesafirishwa kwa lazima kutoka nchini Kenya na ambaye ana uraia wa Canada alijitangaza kwamba ni kinara wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM).

Aliandika ujumbe wa kumdunisha Joho katika tangazo la kujulisha watazamani wa Runinga ya Citizen kwamba Gavana huyo angehojiwa katika usiku huo saa tatu.

Katika ujumbe huo kupitia akaunti ya Twitter, Bw Miguna alimpuuzilia mbali Bw Joho ambaye ni naibu kiongozi wa ODM, akimtaja kama ambaye amefeli katika majukumu yake.

“Hahaha! Inachekesha. Kutoka mume wa kijamii (community husband) hadi Gavana aliyepata alama ya D-, stori ya Wakenya wawili ambao wamepungukiwa kimawazo,” akaandika Miguna.

Kauli ya Miguna ilikawakasirisha wafuatiliaji habari mitandaoni (netizens) waliomwonya dhidi ya kumtusi Joho.

Wengine walimtaka kuelezea jinsi elimu yake ya juu imemsaidia.

Sam Kiptoo akamuuliza: “Hahaha! Joho anahudumu muhula wake wa pili akiwa gavana lakini wewe mbona PhD yako haikukusaidia kushinda ugavana katika kaunti ya Nairobi mnamo mwaka 2017?

Fredrick Otieno naye akaandika: “Umekuwa msumbufu zaidi. Tafadhali jaribu kuwaheshimu watu wengine hata kama mwatofautiana kimawazo. Nawe utaheshimiwa hata huko Canada ulikotorokea.”

Kwa upande wake Rashid Mark alisema, “Upende usipende, sharti utahitaji kushirikiana na watu kama hao ambao walipata alama za D ili uendeleze ndoto zako za kisiasa. Ukiwa na fikra kama hii, itakuwa vigumu kwa Wakenya kukupigia kura.

Hata hivyo, Bw Miguna alieleza kuwa hamchukii Joho kwani ni “ukweli kwamba alipata D- masomoni.”