Makala

2022: Cheo kipya cha Oparanya kitang'arisha nyota yake kisiasa?

January 23rd, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

KUCHAGULIWA kwa Gavana wa Kakamega Wycliffe Ambetsa Oparanya kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) kumemweka katika safu ya juu katika siasa za kitaifa huku ushawishi wake ukitarajiwa kuimarika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema wadhifa wake mpya utaimarisha nafasi yake ya kuwania urais au kupewa cheo cha juu katika serikali itakayobuniwa na yule atarithi kiti hicho baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu.

Bw Oparanya, ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha ODM, ametangaza kuwa atawania urais katika uchaguzi mkuu ujao baada ya kukamilisha muhula wake wa pili na mwisho kama gavana wa Kakamega. Sawa na rais, katiba ya sasa haiwaruhusu wagavana kuhudumu katika nyadhifa hizo kwa zaidi ya mihula miwili.

“Ushindi wa Gavana Oparanya utamfaidi pakubwa kisiasa katika miaka ijayo ikizingatiwa kuwa tayari analenga cheo cha juu baada ya kukamilisha hatamu zake katika uongozi wa kaunti ya Kakamega. Rekodi yake ya maendeleo ambayo pia ni ya kupigiwa mfano huenda ikampiga jeki hata zaidi na kuimarisha ndoto zake katika ulingo wa siasa,” anasema Bw Martin Andati.

Lakini mchanganuzi huyo wa masuala ya siasa anaongeza kuwa itamlazimu Bw Oparanya kukabiliana na mawimbi makali ya kisiasa kutoka kwa kiongozi wa chama cha Amani National Congresss (ANC) Musalia Mudavadi na kiongozi wa chama chake Raila Odinga ambao wana ushawishi mkubwa katika uliokuwa mkoa wa magharibi anakotoka.

“Ni kweli kwamba Bw Oparanya ametangaza nia yake ya kuwania urais 2022. Lakini hata akikosa kuwania wadhifa huo kutokana na mabadiliko ya kisiasa ambayo huenda yakajiri kuelekea uchaguzi mkuu ujao, wadhifa huu utaimarisha hadhi yake kisiasa kiasi kwamba wagombeaji wengine wa urais watataka kubuniwa ushirikiano naye,” anaeleza Bw Andati.

Kauli ya Bw Andati inaungwa mkono na Dkt Adams Oloo ambaye anashauri Bw Oparanya kucheza karata zake za kisiasa vizuri ili aweze kufaidi kisiasa kutokana na wadhifa wake mpya, walivyofanya watangulizi wake Isaac Ruto (aliyekuwa Gavana wa Bomet) na Peter Munya (Meru).

Nyota ya Bw Ruto aliing’aa kisiasa alipohudumu kama mwenyekiti wa CoG kwa mihula miwili hali iliyomwezesha kubuni Chama cha Mashinani (CCM) alichotumia kujiunga na muungano wa NASA. Naye Bw Munya alitwaa uongozi wa chama cha PNU baada ya kuhusu kama mwenyekiti wa CoG kwa vipindi viwili.

Baadaye aligeuka kuwa kivutio cha mirengo ya Jubilee na NASA licha ya kushindwa kadumisha kiti chake katika uchaguzi wa 2017, hali iliyochangia kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Biashara katika serikali ya sasa.

Hata hivyo, Dkt Oloo ni mhadhiri wa katika Chuo Kikuu cha Nairobi, anatilia shaka uwezekano wa Gavana Oparanya kutumia cheo hicho kufanikisha ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022.

“Kuanzia sasa Bw Oparanya atakuwa akiketi meza moja na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kujadili masuala yanayohusu ushirikiano kati ya serikali kuu na zile za kaunti. Isitoshe, atakuwa akiketi katika safu moja na Bw Ruto ambaye ni mwenyekiti wa Baraza Shirikishi la Bajeti na Masuala ya Uchumini (IEBC) kutetea nyongeza ya ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti,” anaeleza Dkt Oloo ambaye pia ni mtaalamu wa Sayansi ya Siasa.

Baraza la IBEC hushiriskisha Mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) Spika Justin Muturi, Jaji Mkuu David Maraga ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) na wawakilishi kutoka Tume ya Utumishi wa Umma (PSC), Tume ya Ugavi wa Rasilimali (CRA), Msimamizi wa Bajeti (CoB) kati ya wengine. Mada kuu ya vikao vya baraza hii huwa ni kujadiliwa mikakati ya ugavi wa fedha kati ya ngazi mbili za serikali.

Bw Oparanya alitangazwa mwenyekiti mpya wa CoG baada ya uchaguzi uliofanyika katika mkahawa mmoja jijini Nairobi Jumatatu wiki jana. Na wadhifa wa Naibu Mwenyekiti ulimwendea Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria baada ya aliyeshikilia cheo hicho Bi Anne waiguru kushindani kiti cha mwenyekiti na kupoteza. Wadhifa wa kiranja ulimwendea gavana wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana.

Wengine waliangushwa na Bw Oparanya ni aliyekuwa mtangulizi wake, Gavana Josphat Nanok (Turkana) aliyatetea kiti hicho, Gavana Jackson Mandago (Uasin Gishu), Profesa Anyang’ Nyong’o (Kisumu) na Salim Mvurya (Kwale).

Bw Mvurya, ambaye hakuhudhuria mkutano huo, hata hivyo alipinga uchaguzi huo na kutawazwa kwa Oparanya akisema kwa shughuli hiyo iliendeshwa kinyume na makubaliano ya Desemba, 2017 kwamba yenye ndiye alipasa “kupewa” wadhifa huo.

Hata hivyo, kauli hiyo ilipuuziliwa mbali na Bw Oparanya pamoja na magavana wengine waliosema kuwa kauli ya Bw Mvurya (Gavana wa Jubilee) haijapewa nafasi katika sheria ya usimamizi wa serikali za kaunti, haswa kipengee kinachohusu uchaguzi wa vingozi wa CoG.

“Malalamishi ya mwetu Mvurya hayana mashiko kwa sababu hakuna sheria yoyote inatulazimisha kuheshimu makubaliano yoyote ambayo yalifikiwa nje ya sheria zinazoongoza usimamizi wa baraza la magavana,” akasema Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja (Wiper).

Vile vile, kuna nadharia inayosema kuwa uchaguzi wa Bw Oparanya ulipata ushindi kutokana na maufaka wa maelewano wa kisiasa katika ya Rais Kenyatta na Bw Odinga uliotiwa saini mnamo Machi 9, mwaka jana.

Duru zasema kuwa huenda viongozi hao wawili ndio walitumia ushawishi wao kuhakikisha kuwa CoG inaongozwa na gavana huyo wa Kakamega ambaye amekuwa mtetezo sugu wa mwaka huo, almaarufu, handisheki.

“Ikiwa ni madai hayo ni kweli basi huenda nyota ya Bw Oparanya ikang’aa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 ikizingatiwa kuwa Rais Kenyatta na Bw Odinga bado watashawishi mkondo wa siasa nchini wakati huo,” akasema Bw Andati, bila kutoa ufafanuzi zaidi.