Habari MsetoSiasa

2022: Hatuna deni la kumlipa Ruto, yasema Jubilee

December 27th, 2018 2 min read

DERRICK LUVEGA na VALENTINE OBARA

NAIBU Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee, Bw David Murathe, amepuuzilia mbali shinikizo la wandani wa Naibu Rais, William Ruto kutaka jamii ya Mlima Kenya itangaze itamuunga mkono kuwania urais 2022, na kusema hapakuwepo maelewano kama hayo.

Akizungumza Jumatano wakati wa sherehe za kitamaduni za jamii ya Wamaragoli katika Kaunti ya Vihiga, Bw Murathe alisema kama kulikuwa na maelewano yoyote pengine ilikuwa ni kati ya Rais Uhuru Kenyatta kibinafsi na Bw Ruto.

Bw Murathe alionekana kushawishi jamii ya Waluhya kuungana kisiasa na wenzao wa Mlima Kenya kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Murathe, ambaye husemekana kuwa mwandani wa Rais Kenyatta, aliandamana na aliyekuwa Mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando katika hafla hiyo, siku chache baada ya viongozi wa Mlima Kenya kukutana na Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Bw Musalia Mudavadi faraghani jijini Nairobi.

“Kama Ruto ana maelewano na Uhuru Kenyatta, hayo ni kati yao. Leo tumekuja hapa kuona kama mna umoja. Tunawaomba muunganishe vyama vyenu vya Ford Kenya na ANC kisha tujadiliane,” akasema.

Bw Murathe alizidi kusema Bw Ruto hafai kuwania urais 2022 kwa vile amehudumu mara mbili mfululizo kama naibu wa rais chini ya Rais Kenyatta, ilhali katiba inaruhusu marais kuwa mamlakani kwa awamu mbili pekee.

“Kama umeongoza pamoja na Uhuru kwa awamu mbili, unataka nini tena? Tutachagua mtu ambaye atalinda masilahi yetu kama jamii ya Mlima Kenya,” akasema Bw Murathe.

Wandani wa Bw Ruto wamekuwa na wasiwasi kwa muda mrefu mwaka huu kwamba huenda Rais Kenyatta hatamuunga mkono Bw Ruto ifikapo 2022, hasa baada ya kuweka mwafaka na Bw Odinga mnamo Machi na wandani wake wakuu wakionekana kutaka kuvutia viongozi wote wakuu wa upinzani upande wao.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Rais Kenyatta alikuwa akisisitiza kuwa atamuunga mkono Bw Ruto kuwa rais hapo 2022. Lakini matukio ya kisiasa baadaye yamefanya wandani wa Bw Ruto kuzua shaka.

Katika siku za hivi majuzi, Bw Mudavadi amekuwa akikumbwa na shinikizo kali kulegeza msimamo wake wa kusimama katika upinzani wakati ambapo vinara wenzake wa NASA, ambao ni Kiongozi wa ODM Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka, wanashirikiana na rais.

Bw Mudavadi amekuwa akisisitiza hatajiunga na serikali bali ataendelea kusimama kidete katika upinzani.