2022: Joho awakashifu wanaokejeli azma yake

2022: Joho awakashifu wanaokejeli azma yake

Na SIAGO CECE

GAVANA wa Mombasa Hassan Joho amewakashifu viongozi wa Pwani wanaotilia shaka uwezo wake wa kuwania urais 2022.

Akizungumza siku moja baada ya mkutano wake na magavana watatu wa Pwani katika Kaunti ya Taita Taveta, Bw Joho alisema kamwe hataruhusu kiongozi yeyote kutoka Pwani kumchafulia jina kisiasa.

“Wanapaswa kujua kwamba nimejitayarisha vilivyo wakati huu na eneo la Pwani liko tayari. Wale watu wanaoeneza uvumi hapa na pale wanapaswa kujua nimepiga hatua kubwa na kutimiza mengi ambayo hawajaweza. Nitapigania nafasi hiyo,” akasema Bw Joho.

Aliwarai wenyeji wa Mombasa kuiunga mkono ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), akisema itapeleka maendeleo katika maeneo ya mashinani.

Alikuwa akihutubu katika eneo la Likoni, baada ya kutoa hundi za basari kwa wanafunzi wanaofadhiliwa masomo yao na mpango wa Hazina ya Elimu. Mpango huo unaendeshwa na serikali ya kaunti hiyo.

Bw Joho alisema wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ na siasa zao za ‘mahasla’ hawatawasaidia wenyeji kwa namna yoyote ile.

Gavana huyo alimtaja Naibu Rais William Ruto na waandani wake kuwa maadui wa eneo la hilo na nchi nzima kwa jumla. Aliwaeleza kuwa kundi hilo halina ajenda wala mwelekeo wowote kwenye kampeni zake.

“Hatuwezi kumruhusu mtu ambaye amekuwa serikalini tangu 2013 kuja kuwadanganya watu wetu eti atainua maisha yao kwa siasa za ‘wilbaro.’ Akiwa serikalini, amekuwa pia akisimamia wizara muhimu. Unawezaje kuvuka feri kwa wilbaro?” akashangaa.

Alisema kuwa kama mwaniaji, atazuru katika maeneo mengine na kuwaahidi wakazi kuhusu ahadi atakazozitimiza. Alisema yeye anaruhusiwa kufanya hivyo, kwani atakuwa mwaniaji mpya. Hata hivyo, aliwatahadharisha wenyeji dhidi ya kukubali kudanganywa na wanasiasa.

Wakati huo huo, mbunge Mishi Boko (Likoni), ambaye pia alihutubu katika hafla hiyo, alimuunga mkono Bw Joho kuwania nafasi hiyo, akiwaambia wapinzani wake kujitayarisha kwa wimbi jipya la kisiasa Pwani, kwani watakuwa na mwakilishi wao.

“Tunataka kuwa miongoni mwa wale wanaogawana mamlaka na uongozi wa kitaifa nchini. Tunafurahi kwamba kuna juhudi za kuwaunganisha wenyeji wa Pwani. Wakati huu, tungetaka sauti zetu kusikika kitaifa,” akasema.

Mbunge huyo, anayetajwa kuwa miongoni mwa wale wanaolenga kumrithi Bw Joho, alisema chama cha ODM kimebuni utaratibu wa wazi kuhusu utoaji tiketi kwa wale wanaolenga kuwania urais.

Alisema Bw Joho atatuma maombi ili kujaribu bahati yake.

“Ni wakati wetu pia. ODM ni chama kinachozingatia demokrasia. Kiongozi wetu (Raila) amekubali kuwapa nafasi baadhi ya wanachama wake kutafuta nafasi hiyo. Hatutapoteza muda. Tutafanya lolote tuwezalo kuhakikisha tumemuunga mkono Joho hadi mwisho,” akasema.

You can share this post!

Liverpool kusajili Florian Neuhaus kuwa kizibo cha...

Corona yasukuma watoto kushiriki katika ugaidi – UN