HabariSiasa

2022: Masaibu ya Ruto yaongezeka Kalonzo akiungana na Moi

June 10th, 2019 2 min read

KITAVI MUTUA na CECIL ODONGO

KIONGOZI wa chama cha Wiper Jumapili alitangaza kushirikiana kisiasa na kinara wa KANU Gideon Moi, hatua ambayo imeongeza idadi ya wanaopigana kuvuruga ndoto ya Naibu Rais William Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022.

Hapo jana, Bw Musyoka alifichua kuwa Rais Mstaafu Daniel arap Moi ndiye aliyemshauri kuhusu ushirikiano anaopaswa kufuata katika maazimio yake ya kuongoza nchi ifikapo 2022.

Bw Musyoka alisema alipomtembelea Mzee Moi nyumbani kwake Aprili, rais huyo mstaafu alimwambia ashirikiane na mwanawe Gideon na Rais Uhuru Kenyatta. Gideon ambaye pia ni Seneta wa Baringo na kinara wa KANU ni adui mkubwa wa Naibu Rais William Ruto hasa katika siasa za eneo la Rift Valley na hivyo ushirikiano wake na Bw Musyoka unaongeza presha zinazomkabili Naibu Rais.

Mwishoni mwa wiki kundi la wazee wa jamii ya Agikuyu walikutana Nyeri na kutangaza hawana deni la Dkt Ruto kwa kuunga mkono Rais Kenyatta 2013 na 2017.

Pia anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa chama cha Raila Odinga cha ODM na kundi ndani ya Jubilee linalojiita “Kieleweke”.

“Tulipomtembelea mzee kwake aliniambia ‘fanya kazi na kijana yangu na Rais Uhuru Kenyatta’. Hayo yalikuwa maneno ya kipekee japo hakuniambia jinsi ya kufanya na kupanga kikosi lakini hilo tutajua mbele,” akasema Bw Musyoka wakati wa harambee katika Kanisa Katoliki la Muthale, Kaunti ya Kitui.

Seneta Moi ameibuka kuwa mojawapo ya vikwazo vinavyomtatiza Bw Ruto katika azimio lake la kumrithi Rais Kenyatta ifikapo Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw Moi alithibitisha matamshi hayo ya Mzee Moi na akasema yuko tayari kufanya kazi na Bw Musyoka kuelekea uchaguzi wa mwaka wa 2022.

“Tutaamua vile tutafanya kazi pamoja jinsi mzee alivyoamrisha. Mambo ya 2022 ni ya Mungu japo nakuhakikishia Bw Kalonzo kuwa wewe na mimi tuna nia moja, na wewe ni mtu mwenye maadili asiyetiwa doa la ufisadi. Wakati ukifika tutanyoosha mambo lakini kwa sasa tufanye kazi,” akasema Bw Moi.

Aliongeza: “Nimefika hapa kama rafiki ya jamii ya Wakamba, na nilikuomba ruhusa ili nifanye kazi na viongozi wenu 2022 na ukakubali. Tumetoka mbali hasa jamii zetu mbili. Ukiniona hapa tunarejelea ule ushirikiano wa awali na tumeamua kuwafanyia wananchi kazi na kutimiza ahadi tuliyowapatia.”

Bw Musyoka pia alirejelea kumbukumbu za zamani kuhusu jinsi Mzee Moi alivyomfaa kisiasa na akamtaja kama aliyetabiri uongozi wa Rais Kenyatta licha ya wanasiasa wengi akiwemo yeye kukihama chama cha KANU kutokana na tofauti kuhusu uteuzi wa mwaniaji wa urais mwaka wa 2002.

Wawili hao pia walipigia debe ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga huku Bw Musyoka akiahidi kwamba viongozi wote wa upinzani sasa wanaunga muafaka huo.

Pia walikemea ufisadi na kusema noti mpya zilizozinduliwa zitasiaidia kufanikisha vita dhidi ya ufisadi hasa kwa wafisadi ambao wamekuwa wakificha mamilioni ya fedha kwenye makazi yao.

“Ufisadi ni adui wetu nambari moja na hatufai kukata tamaa. Kuzinduliwa kwa noti mpya kunaonyesha kwamba serikali inafanya mambo kwa uwazi na kila moja wetu lazima aunge mkono,” akaongeza Bw Moi.

Viongozi waliohudhuria hafla hiyo hasa kutoka jamii ya Wakamba pia walisifu ushirikiano wa Bw Musyoka na Bw Moi na kuunga wito wao wa kukomeshwa kwa siasa ili wananchi wapewe huduma za maendeleo.