HabariSiasa

2022: Puuzeni porojo kuwa ninashirikiana na Ruto – Kalonzo

December 12th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka amepuuzilia mbali madai kuwa ameanzisha mazungumzo na Naibu Rais William Ruto kwa ajili ya kujiandaa kuwania urais mwaka wa 2022.

He inafuatia kauli ya aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama Jumatano kuwa ataongoza mazungumzo kwa lengo la kuundwa kwa muungano wa kisiasa kati ya Dkt Ruto na Bw Musyoka kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Muthama alisema katika mahojiano katika redio ya Kikamba Musyi FM akisema kuwa jamii ya Wakamba kamwe haitamuunga mkono tena kiongozi wa ODM Raila Odinga katika uchaguzi mkuu ujao.

Hata hivyo, katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa twitter, Bw Musyoka alipuuzilia mbali madai hayo akisema yalitolewa “na watu fulani kwa nia mbaya.”

Alisema kuwa madai hayo yanalenga kusababisha mgawanyiko kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

“Kufuatia madai yaliyotolea majuzi na uvumi kwamba ninashirikiana na Naibu Rais, nataka ufahamike kuwa madai hayo sio ya kweli na yatolewa kwa nia mbaya,” Bw Musyoka akaandika.

“Madai hayo ni sehemu ya juhudi za kuboronga uhusiano kati yangu na Rais Uhuru Kenyatta, lakini zimefeli. Madai yaliyotolewa na watu fulani hayapasi kuhusishwa na mimi,” akaongeza.

Bw Muthama ambaye aliongoza kampeni za Bw Odinga katika miaka ya 2013 na 2017 alisema uhusiano wake jamii ya Wakenya na Bw Odinga umeisha na kwa jamii hiyo haitamuunga mkono atakapopambana na Dkt Ruto.

Hata hivyo, Bw Muthama alisema bado kuna nafasi ya yeye kufanya mazungumzo na vigogo wa muungano wa upinzani, NASA, Musalia Mudavadi na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula.

“Hivi katibu nitaitisha mkutano ya viongozi wote waliochaguliwa wakiwemo wabunge na madiwani, na wachanganuzi wa masuala kuzungumzia suala hilo -la kufufua NASA. Sura yetu na kiongozi wa ODM Raila Odinga umekamilika na tutafanya mazungumzo na Ruto, Mudavadi na Wetang’ula,” akaeleza Bw Muthama.

Alisema kuwa jamii ya Wakamba ina nia kubwa ya kuwa serikalini 2022. Bw Muthama aliongeza kuwa wabunge wote wa Ukamba wanaunga mkono mazungumzo kati ya Musyoka na Dkt Ruto.

Jumanne, Bw Musyoka na Dkt Ruto walinaswa kwenye picha wakizungumza wakati wa Kongamano la muungano wa mataifa ya Afrika, Karibea na Pacific (ACP) pembezoni mwa jumba la Mikutano ya Kimataifa la Jomo Kenyatta (KICC), Nairobi.

Picha hizo zilisambazwa mitandaoni huku baadhi ya waliozifuatilia wakibashiri kuhusu uwezekano wa Musyoka na Dkt Ruto kubuni muungano kumwangusha Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022.