Habari MsetoSiasa

2022: Ruto anavyotumia chakula cha msaada kujitangaza kisiasa

May 25th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Kujitokeza kwa Naibu Rais William Ruto kugawa chakula cha msaada wakati huu wa janga la corona ni mbinu yake ya kuanza tena ziara zake kote nchini katika hatua za kudumisha ushawishi wake wa kisiasa mashinani, wandani wake wamesema.

Dkt Ruto amekuwa kimya tangu serikali ilipopiga marufuku mikutano ya hadhara na ibada alizokuwa akitumia kuwashambulia wapinzani wake.

Kimya chake kimeendelea huku wandani wake wakibanduliwa kutoka nyadhifa za uongozi katika seneti. Kwa muda wa wiki tatu sasa, amekuwa akigawa chakula cha msaada maeneo tofauti nchini kupitia wandani wake na viongozi wa kidini.

Wiki jana, alijitokeza kwa mara ya kwanza katika hafla ya kugawa chakula eneo la Kikuyu, Kaunti ya Kiambu wakati mipango ya kumtimua Prof Kithure Kindiki kama Naibu Spika ilipokuwa ikiendelea lakini hakuzungumzia siasa.

Mnamo Jumamosi, aliwagawia waumini wa Kiislamu mbuzi kusherehekea sikukuu ya Idd Ul Fitir lakini akaepuka siasa.

“Tunaheshimu kujitolea kwa ndugu na dada zetu Waislamu kuombea Kenya tunapopigana na janga la corona,” alisema Bw Ruto kwenye taarifa kupitia mitandao ya kijamii.

Duru zinasema kwamba ingawa Dkt Ruto alikuwa akitumia wandani wake kugawa chakula cha msaada, baadhi yao waliogopa wakihofia kuchukuliwa hatua na maafisa wa usalama.

“Baadhi yao wanaogopa kuandamwa na serikali na hii ndiyo imemfanya Dkt Ruto kujitokeza kugawa chakula hicho,” alisema mbunge mmoja aliyeomba tusimtaje jina.

Kulingana na mbunge wa Belgut, Bw Nelson Koech, Dkt Ruto amekuwa akigawa chakula cha msaada kote nchini na ataendelea kufanya hivyo.

Alisema wandani wake wataanza kutembelea maeneo tofauti nchini kusaidia Wakenya kwa sababu wamegundua wapinzani wao wametumia kipindi hiki cha kukabili corona kumpiga vita Dkt Ruto.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Muungano wa vyama vya wafanyakazi, Bw Francis Atwoli, alidai kuwa juhudi za Dkt Ruto hazitamuokoa kisiasa.

Bw Atwoli ambaye amekuwa mstari wa mbele kumpiga vita Dkt Ruto anasema Naibu Rais anaharibu wakati wake kujipendekeza kwa watu.

Seneta wa Nakuru Susan Kihika na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro nao wanasema Dkt Ruto atarudi katika ulingo wa siasa kwa kishindo.Mnamo Jumamosi, Dkt Ruto aliunga mpango wa Rais Uhuru Kenyatta wa kufufua uchumi baada ya janga la corona.

“Tumejitolea kufanya kila liwezekanalo katika uwezo tuliopatiwa na Mungu kuzuia kusambaa kwa corona na msaada wa serikali ya Kenya wa kufufua uchumi utapunguza hasara iliyotokana na janga hili,” alisema na kumtakia afueni aliyekuwa mbunge wa Starehe Askofu Margaret Wanjiru aliyeambukizwa virusi hivyo.

Duru pia zilisema jana, Dkt Ruto alikutana na baadhi ya wandani wake kuandaa mikakati ya ziara zake nchini.