Habari MsetoSiasa

2022: Ruto asema yuko tayari kumkabili Raila kisiasa

October 31st, 2018 1 min read

Na MAGATI OBEBO

NAIBU Rais William Ruto Jumanne alimwambia Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga ajiandae kwa mapambano makali endapo atajitoza kwenye kinyang’anyiro cha urais 2022.

Naibu Rais alisema serikali ya Jubilee imejitolea kupiga hatua mbele kimaendeleo akaongeza kwamba “huu ni wakati wa kuchapa kazi wala si wa vitendawili.”

Alikuwa akizungumza katika Kanisa Katoliki la Suneka, eneo la Bonchari, Kaunti ya Kisii aliposimamia harambee.

“Wakati wa mambo ya vyama, siasa na nani anafaa kuwa katika nafasi ipi ulipita na yeyote anayetaka kuwa kwenye shindano anisubiri huko mbele. Mimi siogopi,” akasema naibu rais.

Kulingana na Bw Ruto, serikali imeongeza juhudi zake za kuhakikisha itakamilisha miradi ilizoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita. Alikuwa ameandamana kwenye hafla hiyo na wabunge Oroo Oyioka (Bonchari), Ezekiel Machogu (Nyaribari Masaba), Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini), Alfa Miruka (Bomachoge Chache), Richard Onyonka (Kitutu Chache Kusini) na Innocent Obiri (Bobasi). Naibu Gavana wa Kisii, Bw Joash Maangi pia alikuwepo.

Viongozi hao waliozungumza mmoja baada ya mwingine, kwa kauli moja waliunga mkono azimio la Bw Ruto kutaka kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakayekamilisha hatamu yake ya pili ya uongozi 2022 ambayo ndiyo ya mwisho kikatiba.

Bw Onyonka alimtaka Bw Odinga afafanue wazi sehemu za katiba ambazo anataka zifanyiwe mabadiliko.

Kwa upande wake, Bw Osoro alimwambia naibu rais achague mgombeaji mwenza kutoka Kisii ili ionekane ana imani kwa wakazi wa eneo hilo. Lakini alipinga wito wa viongozi wanaotaka marekebisho ya katiba akasema bado ni mapema mno kuanza kurekebisha katiba ambayo imekuwepo kwa miaka minane pekee.

“Tusionekane kwamba tunafuata misimamo ya mtu ambaye ana lengo la kujinufaisha kibinafsi,” mbunge huyo wa Mugirango Kusini aliambia wakazi.

Bw Maangi pia alizungumzia suala la marekebisho ya katiba na kusema shughuli hiyo inafaa iongozwe na wananchi wenyewe.