2022: Ruto asema yuko tayari kuwania tikiti ya urais Jubilee

2022: Ruto asema yuko tayari kuwania tikiti ya urais Jubilee

Na WYCLIFF KIPSANG

NAIBU Rais William Ruto Jumatano  alisema yuko tayari kumenyana na mwanasiasa yeyote anayetaka kuwania urais 2022 kupitia tiketi ya chama cha Jubilee.

Dkt Ruto alisema wanasiasa wanaotaka kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho ni sharti wajitokeze hadharani na kuipigania badala ya kungojea kupewa.

“Kuna watu wanaotembea huku na huko wakingojea waungwe mkono. Inawezekanaje kuungwa mkono ilhali hauna ajenda yoyote ya maendeleo kwa Wakenya?” akasema Dkt Ruto.

Naibu wa Rais alisema hayo huku kukiwa na mgawanyiko katika chama cha Jubilee.

Baadhi ya viongozi wa chama tawala, wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe, wamekuwa wakimtaka Dkt Ruto kustaafu pamoja na Rais Kenyatta ifikapo 2022.

Bw Murathe alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa, Dkt Ruto hana uwezo wa kuongoza Kenya na akawataka wakazi wa Bonde la Ufa kuteua kiongozi mwingine atakayewania urais 2022.

“Huyu mtu ukimuachia dakika kidogo unaona kile anafanya. Sasa ukipatia yeye hii kiti si kutakuwa kubaya?” Bw Murathe alinukuliwa na gazeti moja la humu nchini jana.

Bw Murathe, ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta, pia alisema hakukuwa na mwafaka wowote baina ya wenyeji wa Bonde la Ufa na wakazi wa Mlima Kenya kuhusu kuunga mkono Bw Ruto baada ya Rais Kenyatta kukamilisha kipindi chake cha mwisho 2022.

Naibu mwenyekiti alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubu wakati wa tamasha la 39 la utamaduni wa jamii ya Wamaragoli mjini Mbale, Vihiga, wiki iliyopita.

Lakini jana, Dkt Ruto aliyekuwa akizungumza alipokutana na wanasiasa kutoka Kaunti za Bungoma na Busia nyumbani kwake eneo la Sugoi, Uasin Gishu, alisema hatatishwa na yeyote na amejiandaa kikamilifu kuingia ikulu 2022.

“Niko tayari kukabiliana na yeyote anayetaka kuongoza nchi hii. Washindani wangu wajitokeze na wataje kile ambacho wametendea Wakenya,” akasema Dkt Ruto.

Naibu wa Rais alisema atawabwaga wawaniaji ambao hawajajiandaa vyema.

Viongozi waliohudhuria mkutano huo wa Sugoi walijumuisha Spika wa Seneti Ken Lusaka, Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong, Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Bungoma, Catherine Wambilianga; na wabunge Didmus Barasa (Kimilili) na Dan Wanyama (Webuye Magharibi).

You can share this post!

Mgomo wa walimu wazimwa

Aliyeingiza mabinti Wapakistani nchini kiharamu akamatwa

adminleo