HabariSiasa

2022: Ruto awawekea mtego wabunge wa Rift Valley wanaompinga

April 21st, 2019 3 min read

CHARLES WASONGA na WYCLIFFE KIPSANG

WABUNGE kutoka Rift Valley ambao wamemuasi Naibu Rais William Ruto huenda wapoteze viti vyao kufuatia njama mpya ya kuwawekea wapinzani, ili wawang’oe kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Wanaolengwa kwenye mpango huo unaosukwa na naibu rais ni pamoja na Alfred Keter (Nandi Hills), Joshua Kutuny (Cherangany), Silas Tiren (Moiben), William Kamket (Tiaty) na Joshua Kandie (Baringo ya Kati).

Watano hao wamejitokeza waziwazi kama wakosoaji wakuu wa Dkt Ruto kwa kutofautiana naye waziwazi kuhusiana na masuala kama vile, vita dhidi ya ufisadi, masaibu ya wakulima wa mahindi, siasa za urithi wa urais 2022, kati ya mengine yenye umuhimu wa kitaifa.

Kuhusu vuta dhidi ya ufisadi, wabunge hawa wakishirikiana na wenzao wa Jubilee na wale wa upinzani, wamemkashifu Naibu Rais kwa kudai vita hivyo vimeingizwa siasa kwa lengo la kuhujumu azma yake ya kuingia Ikulu, 2022.

Na mwezi jana, Kamket, Kutuny na Keter waliungana na kundi la wabunge, maarufu kama, “Kieleweke” kumtaka Dkt Ruto ajiuzulu ikiwa hakubaliani na msimamo wa Rais Uhuru Kenyatta kuhusiana na vita dhidi ya ufisadi.

Duru zasema wandani wa Naibu Rais wanapanga kumwondoa Bw Kutuny kwa “kumsaidia” aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Kipruto Arap Kirwa kutwaa kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao.

Kirwa ambaye pia ni waziri wa zamani wa Kilimo, amewahi kuwakilisha Cherangany kwa miaka 15.

Kulingana na Seneta wa Trans Nzoia, Dkt Michael Mbito, Bw Kutuny amevuka laini katika ukosoaji wake wa Naibu Rais na kwamba, ikiwa hatabadilika atajipata kwenye kaburi la siasa.

“Mkondo ambao Bw Kutuny anafuata bila shaka sio mzuri. Hana heshima kwa naibu kiongozi wa chama chetu. Ingawa hatutaki kuchukua hatua ya haraka dhidi yake, tunataka kumpa nafasi atubu la sivyo atajuta,” Dkt Mbito akasema.

Bw Kutuny, hata hivyo, amepuuzilia mbali mipango ya kumpokonya wadhifa wake 2022 akisema ni haki yake kutoa hisia zake kuhusu masuala yoyote ya kitaifa.

“Naitwa muasi kwa kutetea utawala wa Rais Uhuru Kenyatta?. Kwa hakika yeye, Naibu Rais, ndiye muasi mkubwa ambaye anapaswa kuondolewa kwa kupinga mipango ya serikali. Hatujapungukiwa na viongozi ambao wanaweza kuwakabili waasi kama hao. Tumejindaa kwa mchezo wa siasa kama huo,” Bw Kutuny akasema.

Bw Kirwa ambaye sasa ni Naibu Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), alipuuzilia mbali madai hayo akisema hana habari zozote kuhusu njama hizo.

Naye Bw Keter ameapa kukabiliana kiume na Afisa wa Mawasiliano katika afisi ya Naibu Rais, Bw Emmanuel Talam aliyembwaga alipowania kiti hicho 2017.

“Mimi ni Mbunge wa Nandi Hills hadi 2022 na ni wapiga kura ambao wataamua hatima yangu kisiasa. Watu fulani ndani ya Jubilee wanaojaribu kufurahisha wakubwa wao watashangaa,” Bw Keter akasema. Kwa upande wake Bw Tiren alisema hana habari zozote kuhusu mipango ya kumpokonya kiti cha Moiben na kwamba, ni wapiga kura watakaoamua atakayewaongoza.

Nao Mbw Kamket na Kandie, waliochaguliwa kwa vyama vya Kanu, na Maendeleo Chap Chap, mtawalia wanashikilia kuwa uamunifu wao ni kwa wapiga kura wao wala sio “mtu fulani.”

“Wajaribu tu kuendesha njama hizo. Na ninawakikishia kuwa hawatafauli kwani wakazi wa Tiaty wako na mimi chini ya Kanu,” akasema Bw Kamket ambaye amekuwa akimpigia debe kiongozi wa chama chake, Gideon Moi.

Katika kaunti ya Elgeyo Marakwet, gavana Alex Tolgos pia amejipata pabaya baada ya kujitokeza waziwazi kuunga mkono uchunguzai kuhusu sakata ya wizi wa Sh21 bilioni za ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer, hatua iliyowakasirisha baadhi ya wandani wa Naibu Rais.

Wiki jana, Bw Tolgos, anayehudumu muhula wake wa mwisho, alisema mipango inayoendeshwa ya kuwaondoa afisini baadhi ya mawaziri wake inadhaminiwa na watu ambao hawafurahishwi na msimamo wake kuhusu sakata ya mabwawa hayo.

Mwezi jana, Bw Tolgos aliwakashifu wandani wa Dkt Ruto ambao walimshambulia Rais Kenyatta hadharani kutokana na sakata hiyo ya mabwawa. Gavana huyo alijitokeza na kuomba msamaha kwa Rais kwa “kwa niaba ya wakazi wa eneo letu.”