Habari MsetoSiasa

2022: Ruto hahitaji tiketi ya moja kwa moja ya Jubilee, wandani wamkosoa Tuju

December 31st, 2018 2 min read

Na ONYANGO K’ONYANGO

WANASIASA kutoka jamii ya Wakalenjin Jumatatu walisema kuwa Naibu Rais William Ruto hahitaji tiketi ya moja kwa moja kutoka chama cha Jubilee ili awanie urais mwaka wa 2022.

Walisema Dkt Ruto atashindana na wanachama wengine ambao watajitokeza kutaka udhamini wa chama hicho kuwania wadhifa huo wakieleza kuwa wao, kama wafuasi wa naibu huyo wa rais, wanaheshimu demokrasia.

“Tuju anaweza kuleta mgombeaji anayempendelea bila woga wowote kwa sababu Bw Ruto hahitaji tiketi ya moja kwa moja bali atawashinda wapinzani wake wote,” akasema Mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono.

Mbunge huyo na wenzake walisema hayo siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju kusema kuwa chama hicho hakitampa Dkt Ruto tiketi ya moja kwa moja 2022.

Kauli ya Tuju ilijiri siku chache baada ya naibu mwenyekiti wa chama hicho David Murathe kumtaka Ruto kustaafu pamoja na Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2022.

Akiongea katika hafla ya Kitamaduni ya Wamaragoli katika uwanja wa michezo ya mjini Mbale, Kaunti ya Vihiga wiki jana, Bw Murathe aliongeza kuwa jamii za Mlima Kenya hazina mkataba na Dkt Ruto kwamba zitamuunga mkono kumrithi Rais Kenyatta 2022.

Bw Rono aliwaonya Tuju na Murathe dhidi ya kutumiwa na wapinzani na Naibu Rais wanaolenga kuvuruga ndoto yake ya kuingia Ikulu.

“Wawili hao wakome kutumiwa kuvuruga chama cha Jubilee kwa lengo la kuendeleza matakwa ya maadui wa kisiasa wa Naibu Rais,” Bw Rono akasema.

Mbunge wa Soy Caleb Kositany, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee, pia alipinga madai ya Tuju akisema naibu rais hajawahi kutaka apewe tiketi ya moja kwa moja kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.

“Naibu Rais hajawahi kuomba tiketi ya moja kwa moja na hatuitaki. Tuko tayari kuishindania pamoja na wengine. Tuju hapaswi kutukumbusha kuhusu jambo ambalo ni wazi kwani tunaheshimu demokrasia,” akasema Bw Kositany.

Naye Seneta wa Nandi Samson Cherargei alimwonya Bw Tuju dhidi ya kutoa matamshi ambayo yanaweza kusababisha misukosuko ndani ya Jubilee akisema kuwa Katibu huyo Mkuu anapaswa kutangaza msimamo ambao umefikiwa katika kongamano la wajumbe maalum.

“Tuju anapaswa kukoma kutoa kauli ambazo zinaweza kuleta mgawanyiko katika chama kwani yeye ni afisa mwenye cheo cha juu. Anapaswa kutangaza msimamo wa chama wala sio yale aliyoyasema Jumapili ambayo hayajaidhinishwa na wajumbe,” akasema.

Wabunge hao waliwaunga mkono wenzao kutoka eneo la Kati mwa Kenya ambao wapendekeza uchaguzi wa viongozi wa Jubilee ufanyike ili kuzidisha umoja katika chama hicho.

“Sharti tufanye uchaguzi wa chama kulingana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa ili kufanikisha mipango yake ya siku zijazo,” akasema Bw Cherargei.