2022: Uhuru kujipanga upya

2022: Uhuru kujipanga upya

JUSTUS OCHIENG na RICHARD MUNGUTI

RAIS Uhuru Kenyatta anakabiliwa na wakati mgumu kusukuma mikakati yake ya urithi atakapostaafu 2022, kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kuzima mpango wa BBI.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, Rais Kenyatta alikuwa akitegemea pendekezo la kuongeza nyadhifa za juu serikalini katika juhudi za kumzima naibu wake William Ruto kuwa mrithi wake.

BBI ilikuwa inapendekeza kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu na manaibu wawili, vyeo ambavyo rais alikuwa akivitumia kuwashawishi vigogo wa siasa za kimaeneo kujiunga na muungano mkubwa wenye nguvu za kumzima Dkt Ruto kwenye uchaguzi wa mwaka ujao.

Kati ya walio kwenye hesabu ya kubuniwa kwa muungano huo ni Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (Amani National Congress), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

Mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo anasema uamuzi wa mahakama wiki iliyopita ni pigo kubwa kwa mpango wa Rais Kenyatta kuhusu urithi wa madaraka ya nchi atakapostaafu 2022.

“Ushawishi aliokuwa nao rais kuhusu urithi wake 2022 umefifia. Sasa tegemeo la hesabu yake mpya liko katika matumaini kuwa Mahakama ya Rufaa itatupilia mbali uamuzi wa Mahakama Kuu,” asema Bw Bigambo.

Aongeza: “Rais, Raila na wenzake watalazika kutafuta mbinu mpya ya siasa.”

Mchanganuzi mwingine, Dismas Mokua kwa upande wake anasema mpango wa urithi wa Rais Kenyatta unaweza kufanikiwa iwapo uamuzi wa Mahakama Kuu utatupiliwa mbali.

“BBI ni chombo kimoja ambacho Uhuru anatumia kushawishi matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2022. Anaweza kutumia Mahakama ya Rufaa ama ya Juu kusukuma BBI kwa kufutilia uamuzi wa Mahakama Kuu. Pia anaweza kutumia bunge kufanya marekebisho yasiyohitaji kura ya maoni, ama hata kuachana na BBI kisha kuanza kampeni kana kwamba yeye ndiye anawania urais. Pia anaweza kumwekea vikwazo naibu wake,” asema Bw Mokua.

Kulingana na Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Moi, Rais Kenyatta alifanya makosa kwa jaribio lake la kuongoza mchakato wa urithi wake.

“Mpango wa urithi wa Uhuru umevurigika. Ingekuwa busara kwake kumaliza kipindi chake na kuondoka, kwa sababu ni vigumu sana chini ya Katiba ya 2010 kushawishi urithi wako mwenyewe,” asema Prof Oluoch.

Msomi mwingine Prof XN Iraki wa Chuo Kikuu cha Nairobi anaunga mkono msimamo wa Prof Oluoch, akieleza kuwa kuvurugika kwa BBI kuna uwezo mkubwa wa kuvuruga ndoto za wanasiasa wakuu.

“Kura ya maamuzi kuhusu BBI ni kama mazoezi ya 2022, na wanasiasa wangependa hivyo sana, kwani itawasaidia kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Kura hiyo itafanya 2022 kuwa rahisi kwa mpango wa Uhuru kwani itagawa nyadhifa kuu za kitaifa kwa vigogo. Isipofanyika, ndoto za baadhi ya wanasiasa zitavurugwa,” asema Prof Iraki.

Bw Bigambo anaunga mkono kauli hiyo akisema kuwa bila kura ya maamuzi, wale waliokuwa wanategemea BBI kwa ajili ya 2022 watakuwa katika hali ngumu kisiasa.

“BBI inampatia Uhuru fursa ya kushawishi urithi wake. Bila BBI atajipata katika hali aliyokuwa nayo Mwai Kibaki kwa kubaki kutumia mbinu za kichinichini kusaidia anayetaka kuwa rais, ama awe katika hali ya Mzee Moi ampapo atatangaza mrithi na kusubiri matokeo yake,” asema Bw Bigambo.

Wakati huo huo, ofisi ya mwanasheria mkuu jana ilianza harakati za kukata rufaa ya kupinga maamuzi ya kuharamisha mchakato wa BBI.

Arifa ya kupinga uamuzi huo wa majaji watano iliwasilishwa jana katika Mahakama Kuu huku Mwanasheria Mkuu akiomba nakala za ushahidi ndipo awasilishe kesi katika Mahakama ya Rufaa.

Katika arifa hiyo mwanasheria mkuu alieleza kutoridhika kwake na uamuzi huo wa majaji watano ulitolewa Mei 13, 2021 na kwamba ataomba Mahakama ya Rufaa iubatilishe ndipo harakati za kufanyia katiba mageuzi ziendelee kama ilivyopangwa.

You can share this post!

Vifo vinavyotokana na kufanya kazi kwa saa nyingi...

Ashtakiwa kufanya kitendo cha kipumbavu ndani ya feri