Afya na Jamii

Jogoo wangu amekataa kuwika asubuhi, jambo lililonipunguzia raha chumbani

Na DKT FLO June 17th, 2024 1 min read

Mpendwa Daktari,

Mimi ni mwanamume wa miaka 45. Kwa miezi kadhaa nimekuwa na tatizo la kusimamisha uume wangu hasa asubuhi, huku kiwango cha ashiki pia kikididimia. Tatizo ni lipi?

Karani, Mombasa

Mpendwa Karani,
Kukumbwa na tatizo la kusimamisha uume mara kwa mara hakupaswi kukukosesha usingizi.

Hata hivyo, hali hii ikiendelea huwa ni kwa sababu za kimwili au kisaikolojia.

Huenda una matatizo ya kimwili yanayoathiri uwezo wa kusimamisha uume wako, kwa mfano,kupungua kwa viwango vya homoni za testosterone, matatizo ya neva, maradhi ya moyo, kiwango cha juu cha cholesterol, mishipa ya damu kuziba (atherosclerosis), kisukari, shinikizo la moyo, matatizo ya usingizi, uzani mzito kupindukia, unywaji pombe kupindukia, matumizi ya mihadarati, au maradhi ya peyronie’s (tishu kujiunda kwenye uume.

Pia tatizo hili laweza tokana na masuala ya kisaikolojia kama vile mawazo, wasiwasi, msongo wa akili, matatizo ya kimahusiano na mengine.

Kiwango cha chini cha ashiki inamaanisha kwamba hamu ya kushiriki tendo la ndoa imepungua na hivyo ni ngumu kusimamisha uume.

Muone mwanayurolojia (daktari mtaalam wa mfumo wa mkojo) ili akusaidie kutambua kiini cha tatizo hili na hivyo kupata suluhu.

Haya yakijiri, dumisha lishe bora, fanya mazoezi kila mara, pata usingizi wa kutosha (kati ya saa 7 na 8 kila siku), epuka pombe na sigara na utafute njia za kudhibiti mawazo.

Pia utanufaika kutokana na mazoezi ya pelvic floor ili kuthibitisha misuli katika sehemu ya nyonga.